THOMAS Muller wa Ujerumani ameanza vizuri kampeni yake ya kutetea kiatu cha dhahabu baada ya kupiga mabao matatu (hat-trick) wakati nchi yake ilipoibuka na ushindi wa maangamizi dhidi ya Ureno.
Akiwa na umri mdogo wa miaka 20 katika 'World Cup' iliyopita (2010) Muller ndiye aliyekuwa mshindi wa kiatu cha dhahabu kwa kutupia wavuni mabao matano.
Ujerumani iliifunika kabisa Ureno katika mchezo wa Kombe la Dunia wa kundi G na kama wangekuwa makini wangeweza kuibuka na ushindi mnono zaidi.
Mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo alishindwa kuisaidia Ureno na ilionekana wazi kuwa kikosi hicho kinachonolewa na Paulo Bento kilikuwa na upungufu mkubwa wa wachezaji wenye uwezo wa kubadili sura ya mchezo.
Muller alianza kufunga katika dakika ya 12 kwa njia ya penaliti, kabla hajafunga magoli mengine dakika ya 45 na 78.
Bao lingine la Ujerumani lilifungwa na beki Mats Hummels kunako dakika ya 32.
Hat-trick ya Muller inakuwa ni ya kwanza tangu michuano hii ya Kombe la Dunia 2014 ianze Alhamisi iliyopita.
Beki wa kati wa Ureno, Pepe naye akafanya madudu kwa kufanya faulo ya kijinga iliyopelekea kulambwa kadi nyekundu dakika ya 37 wakati huo matokeo yakiwa 2-0.
Ilikuwa umbali wa mita kama 30 kutoka lango la Ureno, Pepe akawa anachuana na Muller. Beki huyo wa Ureno akaachia kiwiko cha kishkaji, Muller akaenda chini.
Lakini sinema haikuishia hapo, Pepe akaona kama vile Muller amejidondosha kirahisi, akamfuata pale chini na kumparaza kwa kichwa.
Pepe anajua mwenyewe nini kilimtuma afanye vile na refarii Milorad Mazic kutoka Serbia hakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kumlamba beki huyo kadi nyekundu. (Tazama picha za tukio zima hapo chini)
Hii maana yake ni kwamba Pepe hataichezea tena Ureno katika hatua ya makundi.
Germany: Neuer 6; Boateng 6, Mertesacker 6, Hummels 7 (Mustafi 73min, 6), Howedes 6, Lahm 7; Khedira 7.5, Kroos 6; Muller 8 (Podolski 80), Ozil 5.5 (Schurrle 63, 6.5), Gotze 7.
Ureno: Patricio 5.5; Pereira 5, Alves 5, Pepe 2, Coentrao 4.5 (A Almeida 65, 5.5); Moutinho 5, Veloso 5 (Costa 45, 5), Meireles 5; Nani 6, H Almeida 5 (Eder 23, 5), Ronaldo 5.