Friday, June 13, 2014

NHC yavutia wawekezaji katika maonyesho ya Nyumba ya Dubai



NHC yavutia wawekezaji katika maonyesho ya Nyumba ya Dubai

    Makamu wa Rais, Dr Bilal akizungumza kwenye kongamano hilo.
    Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Mchechu akizungumza wakati wa kongamano hilo.
 Wageni waalikwa katika kongamano.

Dubai, United Arab Emirates-Katika kile kinachoonekana ni hatua kubwa katika kuelekea kutengeneza fursa kwenye sekta ya uendelezaji wa makazi, Shirika la Nyumba la Taifa limeweka historia kwenye soko la kimataifa na kufanikiwa kwa mara ya kwanza kufanya kongamano la uwekezaji hapa Dubai ambalo limefanikiwa kufikia lengo lake la kuonyesha fursa zilizopo kwenye sekta ya ujenzi kwa makampuni makubwa ya ujenzi yaliyopo Mashariki ya Kati na kwingineko.
                             
Tukio hili la kipekee na kihistoria kwa Tanzania lilizinduliwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Gharib Bilal na lilihudhuriwa na makampuni makubwa ya ujenzi Dubai kama Damac, Nahkeel, Jumeirah na Emaar, ambayo yamehusika na ujenzi wa majengo makubwa na maarufu Dubai kama Burj Khalifa, Hoteli za Jumeira na Dubai Mall.

Makampuni mengine yaliyohudhuria kutoka ukanda wa Guba kama Qatar na Bahrain pamoja na nchi nyingine kama Korea, Sweden na Romania yameonyesha kuwepo kwa nia ya makampuni makubwa kuwekeza kwenye sekta ya makazi Tanzania.
1

Malengo ya Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa;

Kongamano la Wawekezaji Wa Sekta ya Makazi Tanzania ni sehemu ya lengo kuu la Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Mchechu, ambaye kwa sasa analiongoza shirika hilo kubwa Afrika Mashariki. Kipindi cha Msechu kwenye uongozi kimeonyesha mabadiliko na ubunifu mkubwa kwenye uendelezaji wa sekta ya makazi nchini.

Mchechu anasema lengo kuu la kongamano hili ni hatua kubwa kuelekea mkakati wa kuionyesha dunia kuwa Tanzania ni sehemu pekee likija swala la uwekezaji na urudishaji wa faida kwenye sekta ya makazi.

'Tanzania inatoa fursa ya pekee linapokuja swala la uwekezaji kwenye sekta ya makazi barani Afrika na hii ni kutokana na uwazi pamoja na utulivu wa kisiasa na amani inayopatikana nchini, uchumi unaokua pamoja na ushirikiano mkubwa unaotolewa na serikali' anasema Mchechu.

'Tukio hili la kihistoria ni sehemu tu ya mpango kamili wa kuifahamisha dunia kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya makazi zinazopatikana nchini' alisema Mchechu.
Mchechu anaamini kuwa huu ni muda mwafaka kwa wawekezaji kuitazama Tanzania na Afrika kwa ujumla. 'Zamani ilikuwa ni hatari kwa wawekezaji kuwekeza Afrika na Tanzania, lakini kwa uchumi wa leo, ni hatari kutokuwekeza Tanzania' alisema Mchechu.

Kati ya miradi iliyoonyeshwa kwa wawekezaji ni pamoja na miradi mitatu ambayo itaendelezwa kwa kwa kipindi cha miaka 5. Hii inajumuisha miradi miwili ya kuendeleza Arusha inayoitwa Safari City na USA River ambayo kwa pamoja itakuwa na jumla ya nyumba 8000, pamoja na mradi mwingine wa kuendeleza makazi Dar es Salaam utakaofahamika kama Salama Creek Satellite City ambao utakuwa na jumla ya nyumba 9,500.

Miradi hii yote iko tayari kwa maana ya kuwa vibali vyote vya mradi vimepatikana na kinachotakiwa ni kuwekeza tu, na ndio maana kongamano hili lilikuwa muhimu kwa ajili ya kupata uwekezaji unaotakiwa.


Serikali inatimiza wajibu wake;

Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dr Mohamed Gharib Bilal akizungumza na wageni waalikwa alielezea namna serikali yake imefanya kazi kubwa kwa miaka michache iliyopita kuhakikisha inatengeneza fursa katika sekta ya makazi, ambapo mabadiliko makubwa yalikuwa katika maeneo matatu makuu ambayo sasa yamekuwa sheria. Maeneo hayo ni pamoja na mikopo ya nyumba, uanzishwaji wa kampuni ya kusaidia kuwezesha mikopo ya nyumba (TMRC),pamoja na upitishaji wa sheria ya Condominium ambazo kwa hakika zimechangia mabadiliko makubwa kwenye sekta ya makazi.

'Tanzania kwa sasa inashuhudia mafanikio makubwa kwenye sekta ya makazi, huku kukiwa kuna upungufu wa jumla ya nyumba milioni 3.8 na upungufu huo unakua kwa kiasi cha makazi 200,000 kwa mwaka, ambayo kwa hakika inatoa changamoto kubwa kwa Tanzania lakini ni fursa kubwa kwa wawekezaji' alisema Bilal.

Naye Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Falme za Kiarabu, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na wageni waalikwa alisisitiza namna sekta ya makazi ilivyoimarika nchini Tanzania.

'Sekta ya makazi ndio sekta inayokua kwa kasi zaidi nchini Tanzania na tunakaraibisha wawekezaji kutoka nchi za falme za Kiarabu' alisema Mbarouk.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa George B. Simbachawene, anasema msingi mkuu wa kukua kwa sekta ya makazi ni ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ambao unaruhusu uwekezaji na ukuaji mzima wa sekta.

'Ushirikiano baina ya sekta binafsi na serikali ni muhimu kwa ukuaji wa sekta ya makazi. Tukio kama hili linaruhusu wawekezaji kutoka nchi za falme za Kiarabu kuona fursa zilizopo Tanzania na kuzitumia' anasema Simbachawene.

Kiwango cha Uwekezaji ni kipi?

Mchechu anasema kongamano la hili linalenga kufikia wawekezaji wenye uwezo wa kuanzia dola milioni 20 hadi dola nusu bilioni.

'Tunajua uwezo wa uwekezaji unaotakiwa hauwezi kufikiwa kwa usiku mmoja na ndio maana miradi yetu mingi ni zaidi ya miaka 5 hadi 7, lakini tuna miradi ambayo inaanzia dola milioni kumi hadi dola milioni mia, kwahiyo kiasi chochote ambacho mwekezaji atakuwa nacho kati ya kiwango hicho tuna fursa za kuwekeza' anasema Mchechu.


Watanzania Wanaowekeza Tanzania:

Mchechu anasema kutafuta wawekezaji hakuishii tu kwa wale walio nje ya Tanzania bali hata kwa Watanzania, na kwa kuanza kutakuwa na kongamano mwisho wa mwezi huu litakalofanyika Dar es Salaam ambalo litajumuisha wawekezaji walio nchini wanaotaka kuendeleza nchi yao.

'Hatujasawahau dada na kaka zetu nyumbani Tanzania, wengi wao wana nafasi kubwa ya kuwekeza katika miradi ya uendelezaji wa sekta ya makazi nchi, na tunataka kuhakikisha wanapata fursa hiyo pia' anasisitza Mchechu.

Ushirikiano na Wadau:

Kongamano hili limefanyika kwa ushirikiano kati ya Balozi wa Tanzania Dubai, Mheshimiwa Omary Mjenga pamoja na Balozi Maalumu wa Mambo ya Kiuchumi, Bwana Cleophas Ruhumbika, ambao walishughulikia taratibu za kongamano pamoja na kualika makampuni ya uwekezaji ya Dubai.

"Tuna furaha kubwa kufanya kazi bega kwa bega na Shirika la Nyumba la Taifa kwenye tukio hili la kihistoria' anasema Mjenga. ' Sehemu kubwa ya kazi yetu hapa Dubai ni kuwezesha fursa kwa Tanzania ambayo inaendana na wajibu wetu hapa. Pia tuna furaha kubwa kuwa tukio limekuwa la mafanikio makubwa na nina hakika kuwa fursa zaidi za wawekezaji kuja Tanzania zitazidi kufunguka' anamalizia Mjenga.