Sunday, June 15, 2014

Benki ya wanawake, SUMA JKT kuanzisha kilimo cha kisasa ya umwagiliaji



Benki ya wanawake, SUMA JKT kuanzisha kilimo cha kisasa ya umwagiliaji
BENKI ya Wanawake TanzaniaT (TWB) kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia  SUMA JKT), wamesaini makubaliano ya kufanya mageuzi makubwa ya kilimo cha biashara cha umwagiliaji kwenye ardhi inayomilikiwa na jeshi hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake, Bi.Margareth Chacha, amewaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa ubia huo pia utawanufaisha sana wakulima wadogo wadogo ambao wanayazunguka maeneo ya JKT kwani mazao yao watayauza kwa JKT.

"Makubaliano haya ni hatua muhimu sana katika kuleta mageuzi ya kilimo hapa nchini kwani hata walima wadogo wanaoyazunguka maeneo ya JKT watakuwa na soko la uhakika la kuuzia mazao yao na kuongeza kipato," alisema.

Alisema kilimo hiyo kitachochea moyo kwa wakulima wadogo wa kujikita zaidi katika kilimo. Mazao yanayotarajiwa kulimwa ni mahindi, karanga, Alizeti na kunde.
"Kila kitu kitakuwa kinapatikana kwenye jamii ambazo zinazunguka maeneo ya uzalishaji ya SUMA JKT na hivyo wakazi wa maeneo hayo watanufaika na huduma za kijamii zitakazokuwa zinatolewa," alisema bi. Chacha.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo mtendaji, malipo yote yanayohusiana na mradi huo mkubwa yatafanywa au yatapitia benki yake."Ushirikiano au ubia huu utaiwezesha JKT kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula hapa nchini na kukiuza kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi na hiyo kuleta matokea makubwa chanya kwenye jamii.

Alisema washirika hao wawili yaani (SUMA JKT and TWB)wamedhamiria kuitafsiri za dhana ya kilimo kwanza kwa vitendo na kuchochea kasi ya maendeleo katika sekta ya kilimo hapa chini.
"Kama watanzania wengi wataamua kujihusisha na kilimo cha biashara kwa umakini unaostahili, ni matumaini yangu shilingi ya Tanzania itaimarika sana dhidi ya dola ya Kimarekani," alisema na kuongeza kuwa Tanzania ina fursa tele kwenye kilimo.

Akifafanua zaidi katika makubaliano hayo, Mtaalamu huyo wa maswala ya kibenki na mkurugenzi huyo mtendaji na mwanzilishi wa benki ya wanawake hapa nchini alisema, mchanganuo yakinifu wa kifedha kuhusu mradi huo kwa msimu mmoja SUMA JKT itapata zaidi ya dola milioni 200 za Kimarekani.

Tangu kuanzishwa kwa benki hiyo chini ya miaka mitano,benki imeshawafikia wajasiriamali wengi wanawake na vijana hapa nchini. Imeshatoa mikopo inayofikia zaidi ya shilingi bilioni 20 katika kuunga mkono ukuaji wa biashara zao.