Tuesday, May 20, 2014

RIPOTI YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIKALI

 
 
 
 
image043
Maelezo –Zanzibar                                                                    20/5 2014
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetakiwa kutoa elimu kwa wananchi ili kujua umuhimu wa utalii nchini na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inatoa  huduma iliyobora   na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha Ripoti ya Kamati ya Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi  Zanzibar kuhusu Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015 Mwenyekiti wa Wenyeviti Hamza Hassan Juma amesema ni muhimu kwa Serikali kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya utalii na kuondosha vitendo vya uahalifu ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaimarika.Amesema ipo haja  Serikali kuimarisha miundombinu itakayowawezesha watalii kupata huduma bora wanapoingia nchini ikiwemo kuimarisha viwanja vya ndege, bara bara, kuongeza vivutio vya utalii na maeneo ya kutembezea watalii, kuweka miji katika hali ya usafi pamoja na kuimarisha ulinzi."Kwa kuwa nchi yetu inategemea zaidi mapato yake kutokana na utalii, bado hatujaekeza ipasavyo katika kutoa taaluma ya kutosha kwa ngazi zote, Chuo chetu cha Utalii  hakijaweza kutoa Shahada  kwa wahitimu jambo linalosababisha nafasi za juu katika ngazi ya ajira kuchukuliwa na wageni na vijana wetu kubakia katika ngazi za chini", alieleza Mhe. Hamza.

Aidha Kamati hiyo imeitaka Serikali kudhibiti ujenzi uanaoendelea maeneo ya Mjimkongwe kwani umeanza kupoteza uasilia wa majengo yake kwa kujengwa majengo ya kisasa jambo ambalo linaweza kuiondoa Zanzibar kwenye miji yenye Urithi wa Kimataifa.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo ameomba Serikali kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili  kuyalinda maeneo yote ya kilimo pamoja na kuyaongezea wigo wa ruzuku na pembejeo kwa mazao ili kuwahamasisha wakulima kuongeza kilimo na kupunguza nakisi ya uagizaji  chakula kutoka nje.
"Pamoja na Serikali kueleza kuwa uchumi wetu unatarajia kuimarika katika mwaka ujao kwa kuimarisha mazingira mazuri ya biashara lakini suala hili inabidi kutekelezwa kwa vitendo na sio kwa maneno ya kwenye vitabu tu kwa kupunguza urasimu kwa wawekezaji hasa wazalendo kwa kuwaondolea vikwazo wanapoamua kuwekeza", alifahamisha.
Akizungumzia  mpango wa maendeleo wa Bajeti, Mh. Hamza  ameitaka Serikali kuimarisha huduma za Hospitali za Mjini na Vijijini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja  ambayo ndio kimbilio la wananchi wengi wa  Zanzibar 
Ameeleza kuwa   Hospitali Kuu ya Mnazimmoja,  pamoja na kuwa na madaktari bingwa wa fani tofauti, imekuwa ikipokea wagonjwa wachache  wanaotumia Bima ya Afya ukilinganisha na Hospitali za binafsi.
Amesisitiza kuwa Kamati yake imeitaka Benki ya Watu wa Zaznibar (PBZ) kuanzishe huduma ya kadi ya VISA  na Master ili kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma zake.
"Benki ya Watu wa Zanzibar  wakianzisha huduma hii itaweza kuwavutia wateja wengi hasa wale wakumbwa ambao wengi wao ni wafanya Biashara, "alisema Hamza.
Hamza  Hassan amesema kwa upande wa mapato imebainika kuwa Taasisi zinazokusanya mapato huwasilisha fedha zote katika mfuko mkuu wa hazina jambo ambalo hupelekea Taasisi hizo kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na uhaba wa fedha wanazopatiwa
Kutokana na hali hiyo, amesema kamati yake inazishauri  Serikali kuzipatia Taasisi  hizo  aslimia ya makusanyo yake ili ziweze kutekeleza changamoto zinazowakabili.
"Tunaomba Taasisi kama hizo, aidha zipangiwe utaratibu wa kupatiwa asili mia fulani yaani Retaintion ili ziweze kujimarisha na kujenga uwezo wa kukusanya zaidi ili kuongeza mapato ya Serikali",alisema  Hamza Hassan.
Ameisisitiza kwa Serikali  kufuatilia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya Taasisi inazozipa ruzuku kwa lengo la kujipunguzia mzigo kwa zile Taasisi ambazo zina uwezo wa kujitegemea.
                                          IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR