Friday, November 02, 2012

Bunge laridhia mipaka ya Gombe kurekebishwa




 Sokwe wa Hifadhi ya Gombe
Sokwe wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe

BUNGE limepitisha azimio la kurekebisha mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma ambapo sasa ukubwa wake utaongezeka kutoka kilometa za mraba 33.74 kufikia 56.

Katika marekebisho ya hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1968 yenye sokwemtu, itahusisha kuondolewa kwenye hifadhi eneo la kilometa za mraba 0.2 lenye makaburi, mashamba na nyumba saba pamoja na kuongezwa ufukwe wenye kilometa za mraba 1.26.

Pia kuongezwa kwa ukanda wa maji wenye ukubwa wa kilometa za mraba 21. Katika maamuzi hayo, hakutakuwa na fidia yoyote.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema marekebisho hayo yataimarisha uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori walio hatarini kutoweka hususan sokwemtu; kuboresha uhifadhi wa bionuwai yakiwamo mazalia, makuzio, makazi, maficho na malisho ya samaki na viumbe wengine wa majini.

“Kuongeza shughulil za utalii kama kuogelea, utalii wa mitumbwi na uvuvi wa burudani na kudhibiti mapato yaliyokuwa yanapotea kutokana na watalii kuona sokwemtu bure,” alisema Balozi Kagasheki.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli aliitaka Serikali kuweka alama ya mpaka wa hifadhi katika eneo la ziwa mara mpaka rasmi utakapojulikana ili kuepusha migogoro baina ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa na wananchi wavuvi.

Akichangia azimio hilo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema katika hifadhi hiyo ya Gombe, watalii wanaotembelea wameongezeka kutoka 700 mwaka 2008 na kufikia 2,600 mwaka jana na kuongeza, “naomba sasa uwanja wa ndege uitwe wa Gombe-Mahale ili kuvutia watalii kuja Kigoma”.

Mbali na Hifadhi ya Gombe, pia Bunge limepitisha azimio la kupandishwa hadhi Pori la Akiba la Kisiwa cha Saanane kilichopo mkoani Mwanza ambapo sasa litatambulika kama Hifadhi ya Taifa ikijumuishwa na visiwa vya Chankende Kubwa na Chankende Ndogo na eneo la maji linalozunguka visiwa hivyo.

Kwa mujibu wa Balozi Kagasheki, hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 2.18 kwa kujumuisha pori la Saanane lenye kilometa za mraba 0.76, visiwa vya Chankende Kubwa na Ndogo vyenye kilometa za mraba 0.1 na eneo la maji linalozunguka visiwa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1.32.

Alisema pori hilo lililoanzishwa mwaka 1964 lilikuwa na lengo la kuhifadhi, kulinda bionuwai na kutoa burudani kwa wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Pori hilo lina mimea, wanyamapori waishio majini na nchi kavu na mandhari ya miamba na majabali makubwa.