JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo, imemtia mbaroni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam,Sheikh Issa Ponda Issa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi kanda maalum,Suleiman Kova, alisema kuwa Ponda amekamatwa kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo uchochezi dhidi ya Serikali iliyoko madarakani.
Makosa mengine ni uchochezi wa udini kati ya waislamu na wakristo na ndani ya waislamu wenyewe,kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani jijini.
Tuhuma nyingine ni kulazimisha watu kufanya maandamano hasa wanawake na watoto,kumtisha kumuua sheikh Mkuu Mufti Issa Shaaban bin Simba, kujisifia kuingia Makao Makuu ya Jeshi la Polisi bila ruhusa na uvamizi wa kiwanja.
Tuhuma nyingine ni kuingilia uhuru wa Mahakama, umwagaji wa damu, uchomaji wa makanisa zaidi ya nane, uharibifu wa magari, wizi, upotevu wa vifaa vya makanisa. "Sheikh ponda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola na kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai watuhumiwa waliokamatwa kwa uvunjaji wa makanisa na kufikishwa Mahakamani waachiwe mara moja kabla ya siku saba"alisema.
Ponda alikamatwa juzi majira ya saa 4:30 usiku akiwa kwenye pikipiki kuelekea katika maficho yake maeneo ya Temeke.
"Juzi usiku sijalala kabisa kuhakikisha oparesheni ya kumkamata inakwenda salama, Ponda ni mjanja sana ila Serikali ina mkono mrefu kabla ajaingia katika maficho yake Temeke,alijaribu kukimbia ili atoroke lakini akakamatwa"alisema.
Kova pia alisema kuwa mnamo Oktoba 12,mwaka huu Ponda aliwaongoza wafuasi wake na kuvamia kiwanja namba 311/2/4 block T chang'ombe mali ya kampuni ya Agritanza kwa madai ya kulikomboa.
"Ponda akiwa na wafuasi wake walivamia kiwanja hicho cha agritanza na kudai kuwa wanakomboa mali za waislamu zilizouzwa na Bakwata,uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kiwanja hicho kina hati miliki namba 93773 iliyotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na mikataba mbalimbali ya kuuziana"alisema
Aidha Kova alisema kuwa uongozi wa Bakwata ulipeleka mashahidi kuthibitisha uhalali wa kiwanja hicho na kusema kuwa watu waliovamia wanakabiliwa na shitaka la kuingia kwa jinai pamoja na uharibifu wa mali.
"kati ya watu 38 tuliowakamta wanawake ni saba na wanaume ni 31 na tuliwakuta na silaha mbalimbali kama visu,mapanga,sururu na vifaa vya kuvunjia na vya ujenzi,jenereta na kujenga jengo la haraka"alisema Kova.
Aidha Jeshi la Polisi limesema kuwa limemvumilia Ponda kwa muda mrefu na kuwataka watu wanaoandamana kinyume cha taratib kuacha. "Nawasifu sana wakristo ni wavumilivu,wanabusara kwa tukio la mbagala la kuchoma makanisa la sivyo hali ingekuwa ya hatari na hata hivyo Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu haijasajiliwa kisheria"alisema.
Kova amewataka wafuasi wengine wajisalimishe kwani opareheni inaendelea na watawachukulia hatua za kisheria. Pia amewaasa wananchi kutumia akili zao binafsi na kuacha kufuata mkumbo watashughulikiwa.Jeshi la Polisi linatarajia kumfikisha Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.