Watu wanane wenye silaha zikiwamo za jadi wameliteka basi la abiria la Sumry baada ya kuweka kizuizi cha magogo na mawe katika msitu wa Msaginya kijijini Magamba wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi katika barabara kuu ya Sumbawanga – Mpanda.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, uhalifu huo ulifanyika saa sita usiku wa kuamkia jana ambapo gari hilo lenye namba za usajili T107 BHT lililokuwa likisafiri kwenda mjini Mpanda likitokea mjini Sumbawanga.
Akifafanua, alisema basi hilo lilipofika eneo hilo lenye mteremko na kona kali ambalo lipo kilometa 15 kutoka Mpanda Mjini, lilikumbana na vizuizi vya mawe na magogo ndipo lilipolazimika kusimama ghafla.
Inadaiwa kuwa ndipo walipojitokeza watu wanane waliokuwa mafichoni wakiwa na silaha za jadi zikiwamo mapanga, nondo, mawe na visu na kuwalazimisha abiria wote kushuka ambapo walipekuliwa na kuporwa simu za mkononi 15 na kiwango kikubwa cha fedha, thamani halisi haijafahamika.
Kwa mujibu wa taarifa nyingine kutoka eneo hilo zinadai kuwa baadhi ya abiria walidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo maungoni mwao wakati walipokuwa wakipekuliwa na watu hao ambao kila aliyeshuka garini, alilazimishwa kukabidhi chochote alichokuwa nacho kisha walilazimishwa kulala chini.
Kwa mujibu wa mtoa habari kutoka eneo la tukio ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe alisema baadhi ya abiria walikumbwa na adha hiyo walikuwa wanawake na watoto ambapo mmoja wao alikuwa mtawa wa kike ambaye inadaiwa alikuwa akisafiri kwenda Mwanza.
Hata hivyo, Kamanda huyo alikanusha abiria yeyote aliyevuliwa nguo ila walilazimishwa kulala chini baada ya kuamriwa kushuka garini na gari hilo baadaye liliwafikisha abiria wake hadi Mpanda Mjini.
Kwa mujibu wa Kidavashari kutokana na tafrani hiyo, watu wanane wakiwamo dereva wa gari, Said Chile na utingo wake ambaye jina lake halikufahamika mara moja walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya mjini Mpanda kwa matibabu.
Kamanda alisema Polisi inafanya msako mkali kuwasaka watu hao ambao hadi sasa hawajapatikana na haijulikani walikojificha kwani walikimbia kusikojulikana baada ya kufanya uhalifu huo. (Na Ziro99 blog)