Wednesday, September 19, 2012

MSIGWA AUNGURUMA JIMBONI KWAKE LEO




 Mbunge wa Iringa Mjini kupitia chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) Peter Msigwa leo ameongea na wananchi wake katika eneo la soko kuu la Iringa.

Msigwa akiwahutubia mamia ya watu waliofika katika eneo hilo la mkutano hakusita kuelekeza kilio chake hii ni kutokana na mauji ya kinyama aliyofanyiwa mwandishi wa habari wa channel Ten Daudi Mwangosi mnamo tarehe 2 septemba huko nyororo, Mafinga.

katika mkutano huo msigwa ameshangazwa kuona bado viongozi wa juu katika jeshi la polisi kutojiuzulu kutokana na kuhusika kwa kifo cha mwangosi.

Ameeleza kuwa mwangosi kabla ya kufikwa na umauti alipigwa na polisi ambao wanaaminika katika kulinda wananchi na kuleta amani na kisha kulipuliwa na kufa hapo hapo na kuhoji kwanini wahusika wengine kutoshtakiwa na kuchukuliwa askari mmoja pekee.

"Nashangaa kwanini RPC Kamuhanda yupo katika ofisi mpaka sasa kutokana na yeye kuwa muhusika mkuu katika suala hilo" alihoji

Mbali na hayo amewashangaa viongozi katika ngazi za mkoa kuwa kimya mpaka sasa pasipo kusema lolote kwani marehemu Mwangosi enzi za uhai wake alikuwa akifanya kazi karibu sana na viongozi hao.

Hata hivyo msigwa amewataka wananchi kuwa na subira na kama mpaka Ijumaa Kamuhanda atakuwepo ofisini watafanya maandamano ya amani kushinikiza kujiuzulu kwake kutokana na kile kilichotokea.

Msigwa amewaeleza wananchi kuwa karibu naye na kumweleza kuhusiana na matatizo wanayokumbana nayo ili kwa namna moja ama nyingine ahimize wahusika kuhakikisha wanawapatia huduma nzuri zikiwemo za maji, umeme na barabara.

Katika mkutano huo mbunge huyo akishirikiana na wananchi wameweza kuchangisha kiasi cha zaidi ya milioni mbili kwaajili ya kumsaidia mjane wa marehemu Mwangosi na kutoa jezi na mipira kwa makapteni wa timu mbalimbali za Iringa mjini na kuahidi kuanzisha mashindano ya mpira ambayo yatajulikana kama Msigwa Cup.