Wednesday, September 19, 2012

MFUNGWA HACHAGUI GEREZA SIKUTEGEMEA KUISHI UGENINI IMENILAZIMU......



  Awali ya yote napenda kuwashukuru wote ambao mmeendelea kunitumia ujumbe mfupi katika email yangu hata kupitia simu zangu kunitia nguvu na wale ambao wamekuwa wakipiga simu katika vituo mbali mbali vya radio ambazo nilikuwa nikifanyia kazi hasa Nuru Fm na radio jirani Ebony Fm kutaka kujua afya yangu .

Ukweli nafarijika zaidi na kujiona nipo katika mkoa wangu wa Iringa na nipo katika nchi yangu ya Tanzania inayohubiri amani kila kukicha ila askari wake wanaua kwa mabomu ,sipendi kukumbusha majonzi makubwa ya unyama aliofanyiwa mwenyekiti wangu Daudi Mwangosi ila napenda kusema kuwa mimi ni mzima wa afya njema na familia yangu ambayo kwa sasa tayari imezoea maisha ya ugenini inafanikiwa kupata marafiki kama ilivyo nyumbani Tanzania.

Pia nisingependa kuwa mchoyo wa fadhila kwa kuwashukuru wabunge kama mbunge Peter Msigwa (Iringa) mjini , Ritta Kabati viti maalum mkoa wa Iringa ,Chiku Abwao viti maalum mkoa wa Iringa na mbunge Amina Mwidau viti maalum mkoa wa Tanga pamoja na mbunge wa jimbo la Ismani Wiliam Lukuvi na mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe ambao wamekuwa miongoni mwa wabunge walioweza kunitumia salam za pole kwa yaliyonikuta.

Sina hakika mbunge wangu wa jimbo la Mufindi kusini Mendrady Kigolla jimbo ambalo Daudi Mwangosi aliuwawa kama yupo jimboni kwani binafsi kama mpiga kura wake na tukio likiwa limetokea kwake sijapokea simu wala salam zake kama ilivyo kwa serikali yetu ila simlazimishi pia si vibaya nami kumtakia afya njema mbunge wangu na wengine wote kwa kuwa natambua ni kutingwa na majukumu ya kuwatumikia wananchi .

Ndugu wangu wana Iringa napenda pia kumpongeza katibu tawala wa mkoa wa Iringa Getrude Mpaka ambaye anakwenda kustaafu kwa kunikumbuka mara kwa mara pia mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma ambaye amekuwa akinipigia simu kuwa nirudi nyumbani Iringa na kuwa yeye ni mlinzi wa amani namba moja mkoa wa Iringa nasema ushauri wako mama naufanyia kazi zaidi .

Pamoja na kuwa huku ugenini niliko wakati wote machozi yamekuwa yakinitoka na hata kuwashangaza wenyeji wangu kwa msiba usiokwisha wa Daudi Mwangosi bado nasema sitaacha kutokwa na machozi kwa kifo cha kinyama kilichomkuta Daudi Mwangosi tena mbele ya macho yangu katika Laptop yangu nimeiweka picha yake kabla ya kuuwawa wakati akishambuliwa kwa virungu huku mwenyewe akiwatazama na kutoa tabasamu zito la kuwaaga kama ni sehemu ya ukumbusho wangu na kumuenzi shemeji yangu Daudi Mwangosi mbali ya kuwa mke wangu wakati wote pia amekuwa akilia kwa uchungu na mtoto kuungana na mama yake kulia kabla ya familia nzima kulia ,ila nasema kilio chetu ni sehemu ya kuendelea kumulilia ndugu yetu Mwangosi na sioni vibaya kama tukaendelea kulia wakati wote.

Wosia wangu kwa wanahabari wa mkoa wa Iringa ambao ndio haswa tulishinda na marehemu Mwangosi pamoja ni vema kudumisha umoja na mshikamano na napenda kutumia maneno ya marehemu Mwangosi ambayo siku zote alikuwa akiyatoa katika mikutano na vikao vya Iringa Press Klabu kuwa sitakuwa mtu wa kwanza kuiua IPC nami nasema sitakuwa mtu wa kwanza kuwasaliti wananchi wangu wa mkoa wa Iringa kwa kifo cha Mwangosi nasema popote nitasema kweli na sitasaliti wanahabari wenzangu kwa kupenda pesa kama ilivyo jitokeza kwa kituo kimoja hapo Iringa kwa kusaliti mshikamano eti kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 2 ili kurusha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani .

Ndugu zangu nisingependa kuwachosha kwani hapa nilipo machozi yananitoka hivyo nasema Mungu wabariki wanahabari Tanzania kuwa na mshikamano kama njia ya kulinda heshima yetu,Mungu vibariki vituo vya Radio FM mkoani Iringa kuwa na mahusiano mema na Mungu Ibariki Tanzania na watu wake

Amina