Tuesday, July 03, 2012

KUCHAPISHWA KWA MISIMBO YA POSTA (ORODHA ZA POSTIKODI)



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
Kufuatana na kifungu nambari 41 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapenda kufahamisha umma kwamba orodha ya Misimbo ya Posta au 'postikodi' za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechapishwa kupitia Gazeti ya Serikali Notisi nambari 220 ya tarehe 22 Juni 2012.

Msimbo wa posta (Postikodi) ni mkusanyiko wa tarakimu inayotambulisha eneo la usambazaji wa barua na kwa Tanzania eneo linalotambulishwa ni Kata kwa Tanzania Bara na Wadi kwa Zanzibar.  Kazi hii ya kitaalamu ya kugawa misimbo ya posta imefanyika baada ya utafiti wa muda mrefu ambao umehusisha watalaamu mbalimbali. Ili kuufahamu mfumo wa Msimbo wa Posta wa Tanzania, vigezo vifuatavyo vimetumika kama ilivyofafanuliwa hapa chini.

1.   Ufafanuzi wa mfumo wa msimbo wa posta
Mfumo wa msimbo wa posta wa Tanzania utaundwa na tarakimu tano (5) ambazo zinatafisiriwa kama ifuatavyo:

Muundo wa Msimbo wa Posta
Maelezo


X X X X X

Tarakimu 5 (Mfumo wa Tarakimu za Msimbo wa Posta)
X -  -  -  -
Tarakimu ya kwanza  = Kanda (1 – 7 tazama (a) hapa chini)

X X -  -  -
Tarakimu mbili za kwanza = Mkoa

X X X -  -
Tarakimu tatu za kwanza = Wilaya

X X X X X
Tarakimu zote tano = Kata/Wadi (Eneo la usambazaji)
Tarakimu zote tano = Ofisi ya posta / mteja mkubwa / Eneo maarufu /Misimbo ya posta ya shughuli maalumu.


(a) Tanzania imegawanywa katika kanda 6 na Zanzibar kama ifuatavyo;

1 - Dar es Salaam
2 - Kaskazini
3 - Ziwa
4 - Kati
5 – Nyanda za Juu Kusini
6 – Pwani
7 – Zanzibar

KANDA ZA MISIMBO YA POSTA

(b) Tarakimu ya kwanza na ya pili ya msimbo wa posta (kwa pamoja) inawakilisha mkoa katika Tanzania

(c)  Tarakimu ya kwanza, ya pili na ya tatu (kwa pamoja) inawakilisha Wilaya au Eneo la kati la Biashara katika Wilaya

(d) Tarakimu ya kwanza hadi ya tano ya msimbo wa posta inawakilisha Kata, Wadi, Watumiaji wakubwa wa posta, Vitu maarufu na Shughuli maalumu 

MIFANO YA MISIMBO YA POSTA;

11707: Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
23101: ICC, Arusha
33106: Kirumba, Mwanza
41105: Makole, Dodoma
57103: Mfaranyaki, Songea
63219: Msanga Mkuu, Mtwara
73104: Mkokotoni, Unguja
74209: Wawi, Chake Chake


2.   Vigezo vilivyotumika kugawa misimbo ya posta (postikodi)


Kigezo

Maelezo
1
Eneo la Utawala

Kata au Wadi imechaguliwa kuwa eneo la chini la usambazaji.
2
Ofisi za Posta

Kila Ofisi ya Posta itakuwa na msimbo wa posta. Mteja mwenye S.L.B katika Posta fulani atatumia Msimbo wa posta (postikodi) ya Posta ile.
3
Watumaji wa barua wakubwa

Watumaji wa barua wakubwa kama Wizara za Serikali, Taasisi za Umma, Taasisi za Udhibiti, Makampuni, Taasisi za Kimataifa, Taasisi zisizo za kiserikali zitapewa msimbo maalumu wa posta.
4
Vitu maarufu

Eneo au umbo la kitu ambacho kimehifadhiwa kwa sababu ya kuhifadhi historia litapewa msimbo maalumu wa posta.
5
Matukio au shughuli maalumu  (Kwa muda)

Kutakuwa na misimbo ya posta ambayo itahifadhiwa kwa ajili ya kugawanywa endapo kutakuwa na shughuli maalumu katika nchi.

3.   Anuani mpya zitawezesha ufikishwaji majumbani barua na vifurushi. Kwa mfano anwani kamili inatolewa hapa chini:
Amos Mbawala
20 Barabara ya Mashele
23101 ARUSHA

              2 – Kanda - Kasikazini
                              23 -  Mkoa - Arusha
                                231 – Wilaya - Arusha
                                   23101 –Kata - Sekei

Orodha ya 'Postikodi' imechapishwa kwa ajili ya maeneo ya usambazaji ikijumuisha Mikoa, Wilaya na Kata kama ilivyoainishwa 1 na 2 hapo juu. Orodha ya misimbo ya posta (postikodi) itatolewa kwa ajili ya vigezo vingine vilivyooneshwa 3-5 hapo juu.
Umoja wa Posta Duniani ambacho ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye wajibu wa kuendeleza sekta ya posta katika nchi wanachama, utaarifiwa rasmi ambapo utawafahamisha wadau wakuu wote duniani kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya katika Tanzania. 

Imetolewa:

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
29 June 2012