John Damian Komba.
Na Shakoor JongoMBUNGE wa Mbinga Magharibi Kepteni mstaafu, John Damian Komba anadaiwa kuwa yuko hoi nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu, Risasi Mchanganyiko lina mkoba uliojaa habari hii.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa Mhe. Komba aliondoka nchini wiki iliyopita.
Komba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa za Maonesho la Tanzania One Theatre (TOT) alikwenda nchini humo kwa ajili ya kucheki afya yake lakini amelazimika kufanyiwa upasuaji wa nyonga baada ya kushauriwa na madaktari.
“Awali alikuwa amekwenda kwa lengo la kuangalia afya yake lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi akagundulika kuwa ana matatizo ya nyonga, hivyo akatakiwa kufanyiwa upasuaji haraka sana,” kilisema chanzo chetu kimojawapo.
Mmoja wa ndugu wa karibu na Komba, kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini kwa vile yeye siyo msemaji wa familia, alithibitisha hilo.
Huyu hapa anazungumza: “Ni kweli mzee amekwenda India. Tunashukuru Mungu ameshafanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri. Muhimu kwa Watanzania ni kumuombea dua apone haraka.”