Monday, July 23, 2012

Habari za kina kuhusu kujiuzulu kwa Waziri, Hamad


Habari za kina kuhusu kujiuzulu kwa Waziri, Hamad

Taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee ilisema tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein amekubali ombi la Waziri Hamad Masoud kujiuzulu.

"Tarehe 20 Julai, 2012 Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad alimuandikia barua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohammed Shein ya kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea Julai 18, 2012," ilisema taarifa ya Dkt. Mzee.

Kufuatia kujiuzulu kwa waziri huyo, Rais Dkt. Shein amemteua Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, "Kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rais amemteua Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano," taarifa ya Ikulu ilisema.

Uteuzi wa Waziri mpya wa Miundombinu na Mawasiliano umeanza Julai 23 mwaka huu.

Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Taifa, Profesa Ibrahim Harouna Lipumba amesema hatua ya kujiuzulu aliyoichukua Waziri Hamad inaonesha uwajibikaji wa Kisiasa na Kiserikali kwa viongozi wa chama hicho.

Amesema mfano wa kiongozi huyo kujiuzulu unafaa kuigwa na wakuu wa taasisi za ukozi ambazo zimeonekana kuzorota katika shughuli za ukozi wakati meli hiyo ilipozama

Hata hivyo, Prof. Lipumba amesema hatua ya  kujiuzulu Masoud haimaanishi kuwa anahusika moja kwa moja na uzembe wa ajali hiyo, lakini kwa kiongozi wa kisiasa inapotokea hali kama hiyo katika taasisi zilizoko chini yake anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu. 

Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Waziri Masoud alisema amechukua uamuzi wa kuwajibika kisiasa kwa sababu ajali ya meli hiyo imetokana na hitilafu au utendaji mbaya katika Wizara yake.

Bwana Masoud alisema ingawa yeye hakuwa mtendaji katika operesheni za meli hiyo au usafiri wa baharini, bado anawajibika kama Waziri katika Wizara inayosimamia shughuli hizo.

Alipoulizwa kama ana habari endapo kuna watendaji wengine ambao watajiuzulu au kuwajibishwa, Masoud alisema hayo yatatokana na ripoti atakayopelekewa waziri na tume iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein ameunda Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit.

Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Abdulhakim Ameir Issa, wajumbe ni Meja Jenerali S.S. Omar, COMDR. Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, Salum Taoufiq, Kaptein Hatibu Katandula, Bi. Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla Katibu wa Tume.