Na Walusanga Ndaki
MIAKA 28 imepita tangu aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Julius Nyerere, alipoongoza juhudi za kumng’oa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe. Nyerere alifanya hivyo kutokana na kutofautiana na Jumbe katika masuala yenye kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa kifupi, Jumbe alikuwa ‘amethubutu’ kuhoji muundo wa muungano huo na alikuwa ametayarisha hati mbalimbali kwa ajili ya kulitolea suala hilo ufumbuzi – hasa kwa maslahi ya Zanzibar. Hata hivyo, jambo hilo ambalo wakati wa utawala wa Nyerere lilionekana ni kosa la uhaini. Jumbe aling’olewa urais. Na duru za kuaminika zinasema aliamriwa kuishi Bara na si Zanzibar ambako alionekana angeeneza sumu dhidi ya muungano.
Jumbe ambaye majina yake kamili ni Mwinyi Aboud Jumbe, aliyezaliwa Juni 14, 1920 – miaka miwili zaidi kabla ya kuzaliwa Julius Nyerere – alikuwa rais wa nchi hiyo tangu Aprili 11, 1984 kufuatia kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abeid Karume. Aliishika nafasi hiyo hadi Januari 30, 1984 ambapo Nyerere alimng’oa katika kikao cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika Dodoma.
Hatua hiyo ilimfanya Jumbe apoteze nyadhifa nne alizokuwa nazo ambazo zilikuwa ni: Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.
Ni Aboud Jumbe ambaye amekuwa akiishi Bara tangu tukio hilo na alikuwa rais wa Zanzibar wakati Afro-Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (Tanu) vilipoungana mwaka 1977 na kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
SOURCE(GPL)