Wednesday, May 09, 2012

MSIMAMO WA CCM DHIDI YA TUHUMA ZITOLEWAZO NA CHADEMA

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Nape Nnauye 
---
Hivi karibuni chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilielezea kile ilichoeleza kuwa ni kutishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake.
Madai hayo ya CHADEMA, pamoja na wanachama wengine na mashabiki wao, yalitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, ambaye alidai kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo kwa madai yao imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam Aprili 29 mwaku huu mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mwaka jana.
Mbowe katika maelezo yake alijaribu katika maeneo kadhaa kuihusisha CCM na au serikali yake katika matukio kadhaa yaliyowakabili baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo lile la Mbunge Highness Kiwia ambaye Suala lake bado Lipo mikononi mwa vyombo Vya dola likishughulikiwa.

Katika sehemu kubwa ya maelezo ya Ndg. Mbowe amejitahidi kuonesha kuwa mauaji yote yaliyoikabili na yatakayokuwa yakiikabili Chadema kupitia wafuasi wake yanafanyika kisiasa, Jambo ambalo ni la uzushi, kwani Halina ushahidi wa kisheria hata kimazingira, wa Moja kwa Moja unaoondosha ujinai au makosa hayo, na kuwa ni makosa yanayolenga muktadha wa kisiasa.

Huku akitaka kuuaminisha umma kuwa huo ndio ukweli, Ndg. Mbowe amesisitiza kuwa hilo lime kuwa likitekelezwa na CCM kwa lengo la kuwatisha wananchi kujiunga na chama hicho hoja ambayo haina msingi wowote wa kiutafiti.

Hivyo CCM kwa kutambua kuwa Suala la mauaji linabeba Kosa la jinai, na kwa kuwa Ndg. Mbowe ameshutumu Moja kwa Moja CCM na serikali yake kuihusisha na mauaji hayo, ni vema sasa nasi tukatoa msimamo wetu dhidi ya tuhuma, hiyo.

Kwanza, si busara hata kidogo kuihusisha CCM katika matukio hayo, kwani uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola umeshindwa mpaka sasa kuhusisha matukio hayo na siasa, badala ya kuyahusisha na makosa ya jinai ambayo hufanywa na watu kwa malengo tofauti na yale ambayo Ndg. Mbowe anataka kuwaaminisha watu.

Pili, CCM haijawai, haiwezi, na haitakuja fanya jambo lolote lenye lengo la kuvuruga Amani na Usalama wenye utulivu ndani ya taifa letu, hivyo uzushi na usingiziaji uliofanywa na Mtu Kama Ndg. Mbowe, si vema kuuacha kimya, badala yake nimetumia wasaa Huu muhimu Kujibu, na kutoa ufafanuzi ili Kuupa umma wa watanzania habari sahihi.

Ni aibu kwa Chama kama Chadema kujitahidi kwa nguvu zote kujaribu kuficha ukweli wa mauaji yanayotoa roho za watanzania wenzetu kwa kuyapa sura ya kisiasa. Hizi ni juhudi za makusudi za kutaka kuficha ukweli wa kinachotokea.

Ni aibu kwa chama kama Chadema kujaribu kutumia mauaji mabaya kama haya kutafuta mtaji wa kisiasa. Huku ni kuonyesha jinsi gani wamefilisika kisiasa mpaka wanafikia mahali pa kuamini kuwa wanaweza kutumia chochote kama mtaji wa kisiasa, vikiwemo vifo vya watanzania wenzetu. Huku si kufilisika tu ila kwakweli ni unyama unaotakiwa kulaaniwa na kila muungwana.
 
Imetolewa na:
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM