Elizabeth Michael 'Lulu'.
Haruni Sanchawa na Makongoro Oging'
MAISHA ya msanii maarufu ya filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu'   ambaye yupo katika Gereza la Segerea, yamebainika baada ya gazeti hili   kunasa ukweli jinsi anavyoishi gerezani humo.
 Lulu ambaye anadaiwa   kuhusika na kifo cha aliyekuwa msanii maarufu wa filamu, Steven Kanumba   'The Great' kilichotokea Aprili 7, mwaka huu, imeelezwa kuwa maisha yake   ya mahabusu yanasikitisha.
 Vyanzo vyetu kutoka katika Gereza la   Segerea vinasema msanii huyo licha ya kuwa analetewa chakula kutoka   nyumbani kila siku, huwa anakula baada ya kubembelezwa na baadhi ya   mahabusu wenzake.
 "Lulu siyo yule mnayemfahamu uraiani, humu   gerezani amekuwa mtu wa kusikia kile anachoambiwa na wenzake, amekuwa   msikivu sana na hupenda kulala mara kwa mara," kilisema chanzo hicho.
   Habari zinasema msanii huyo amekuwa akifundishwa aya kwa aya za Biblia   na amekuwa mwepesi kushika baadhi ya mistari ya kwenye kitabu hicho   kitakatifu kwa Wakristo.
 "Bila shaka amekuwa akishika aya kwa kuwa   alizoea kushika maneno yaliyokuwa yanaandikwa katika script za michezo   ya filamu," alisema askari mmoja wa magereza aliyeomba jina lake   kutoandikwa gazetini.
 Alisema kinachosikitisha ni pale anapotembelewa na rafiki zake kwani wakiondoka Lulu hushinda akilia mchana kutwa.
   Aliongeza kuwa hali anayoishi nayo msanii huyo gerezani ni ya kutia   huzuni na simanzi na haonekani kuzoea mazingira kama walivyo mahabusu   wengine.
 Hivi karibuni, ilielezwa kuwa Lulu amekuwa akivaa rosari na   kusoma Biblia mara kwa mara kutokana na mafunzo anayopewa na baadhi ya   walokole waliofungwa katika gereza hilo.
 
