Akizungumza na waandishi wa habari mara baada kutolewa kwa hukumu hiyo, Lema mwaka 2007 aliitwa na kiongozi huyo ili akubali ombi hilo na alimpa watu watakaomsaidia kwenye kampeni zake lakini hakukubaliana naye.Alisema kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 aliitwa tena na kuombwa amuunge mkono mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, ambapo wangemtafutia Lema nafasi ndani serikali, lakini alikataa tena hatua ambayo anaamini ilisababisha chuki.
Aliongeza kuwa sababu nyingine iliyoongeza chuki dhidi yake na serikali, ni hatua yake ya kukataa kushiriki katika mapokezi ya viongozi wa kitaifa waliotembelea Arusha akiwemo Rais Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, na kubwa zaidi kutomtambua meya wa jiji la Arusha Gaudence Lyimo.Katika kuthibitisha madai yake hayo, Lema alisema kuwa alianza kupata taarifa za kushindwa kwake katika kesi hiyo kutoka kwa watu mbalimbali kabla ya hukumu ya jana.
Aliwataja waliowahi kumjulisha kushindwa kwake kuwa ni pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM, maafisa usalama wa taifa na marafiki zake muhimu walioko serikalini.Aliwataja waliomtaarifu kuanguka kwake kuwa ni pamoja na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Mweka Hazina wa chama hicho tawala Mwigulu Mchemba na ofisa usalama mmoja wa ngazi ya juu (jina linahifadhiwa).Alisema kuwa hata walipokuwa kwenye harakati za kampeni jimbo la Arumeru Mashariki Mwigulu Nchemba alisikika akimwambia kijana mmoja aliyeshiriki kura za maoni ndani ya CCM kugombea ubunge jimbo la Arusha Mjini kuwa ajiandae kwa uchaguzi wa Arusha Mjini kwani mahakama itatengua ubunge wake (Lema).“Nilipokuwa najiandaa asubuhi kwenda mahakamani nilipigiwa simu na mbunge wa Kawe Halima (Mdee) ambaye aliniambia amepata taarifa kuwa navuliwa ubunge na katibu wetu mkuu (Dk. Willbrod Slaa) alinipigia kunieleza hivyo hivyo na walinitaka nijipe moyo,”
alisema Lema.
Lema alisema hata alipopita kwenye ofisi yake ya ubunge iliyoko jengo la mkuu wa wilaya alikuta magari ya polisi karibu 10 yaliyokuwa na polisi wengi wenye silaha.Alisema ulinzi mkali na kuzuiwa kwa watu mahakamani kwa kuweka mkanda wa njano kuzunguka majengo ya mahakama, kulithibitisha kuwa tayari watendaji wa serikali na vyombo vya dola walijua kitakachoamriwa.“Kitu walichofanya leo ni cha kusikitisha, maana haiwezekani kesi iliyosikilizwa kwa miezi karibu mitatu jaji akatoa hukumu kwa muda mfupi kiasi kile.
Wao wana dola sisi tuna Mungu,” alisema.Mbunge huyo aliwaambia mamia ya watu waliomsindikiza kwa maandamano kutoka mahakamani hadi zilipo ofisi za CHADEMA mkoa kuwa hukumu hiyo imeendeleza ari yake ya kupigania haki kwa vile ubunge kwake ulikuwa ni utumishi na si vinginevyo hivyo kwa sasa ataendeleza harakati za kudai haki mpaka kieleweke.“Safari ya ukombozi ilianza zamani wengine walikufa wengine walipoteza viungo vyao lakini safari inaendelea, msiogope ninyi mlio wengi, maana mkiogopa mimi nitaogopa zaidi lakini nawatia moyo msiogope kuweni jasiri haki haiwezi kudhalilishwa,” alisema Lema.“Tafsiri niliyoipata mahakamani ni kuwa wametengua matokeo yangu ya ubunge; mtu leo asiumizwe yeyote unayekutana naye leo ni kura yetu, kila mtu ameumia kwa sababu mlipiga kura mkachunga na tukashinda, wao wana jaji wa mahakamani sisi tuna jaji wa mbinguni.”
Source: Jamii Forum