Monday, April 23, 2012

Inatosha: Ubadhilifu Fedha za Walipa Kodi Ukomeshwe!

Taarifa kwa Vyombo vya Habari 22 Aprili, 2012

Inatosha: Ubadhilifu Fedha za Walipa Kodi Ukomeshwe!

Sikika imesikitishwa na kushtushwa na ripoti ya iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha
za Serikali (CAG) iliyoibua matumizi mabaya ya fedha za umma na kiwango kikubwa cha misamaha
ya kodi.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa misamaha ya kodi iliyotolewa imeongezeka kutoka shilingi za Tanzania
bilioni 680.7 mwaka 2009/2010, hadi kufikia trilioni 1.016 mwaka 2010/2011. Ongezeko hili ni sawa
na 18% ya mapato yote yanayotakiwa kukusanywa nchini. Hiki ni kiwango kikubwa ukilinganisha na
majirani zetu wa Kenya na Uganda. Mbaya zaidi, misamaha hii imetolewa kwa watu wenye uwezo na
makampuni makubwa ya kimataifa yenye mitaji mikubwa jambo linalolikosesha taifa mapato.

Fedha zilizopotea kutokana na misamaha hii ya kodi, zingeweza kugharamia rasilimali watu katika
mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya afya uliohitaji kiasi cha shilingi bilioni 500. Katika bajeti
ya mwaka 2011/2012, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilihitaji shilingi bilioni 66.3 ili kuimarisha
rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo ya afya. Cha kustaajabisha, Serikali ilitenga bilioni 13.2 tu na
hadi kufikia Januari mwaka huu ni 20% tu ya kiasi hicho ndiyo iliyokuwa imetolewa. Huu ni mzaha
mkubwa unaofanywa na Serikali, ukilinganisha na upotevu wa fedha uliotokana na misamaha hiyo ya
kodi yenye utata.

Pia, ripoti ya CAG inaeleza kwamba kiasi cha shilingi bilioni 31 zilitumika kununua bidhaa kwa
matumizi ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, huku shilingi bilioni 8 zikitumika bila kufuata
utaratibu maalumu. Aidha, ripoti inaonyesha kuwa shilingi milioni 143 zilitumiwa na serikali kulipa
mishahara kwa wafanyakazi hewa, watoro na waliokwisha staafu.

Wakati huo huo, ripoti inaonesha kuwa shilingi bilioni 1.5 zilitumika pasipo maelezo yoyote na
kuwepo kwa ongezeko kubwa la malipo ya posho. Upotevu wa fedha za umma pia uliongezeka
kupitia madai yasiyoeleweka ambayo yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 11 kwa kipindi cha mwaka
2009/2010 hadi kufikia shilingi bilioni 13 mwaka 2010/2011.

Wakati upotevu huu wa mabilioni ya walipa kodi ukitokea nchini, bado nchi inakabiliwa na matatizo
lukuki ya upatikanaji wa huduma bora za jamii. Mathalan, kumekuwepo na upungufu wa rasilimali
watu katika sekta ya afya, madawa, mfumo mbovu wa usambazaji wa madawa na vifaa tiba pamoja na
uduni wa vifaa vya kutolea huduma za afya.

Ripoti hiyo ya CAG inaonesha matumizi mabaya ya fedha kidogo zinazotengwa kwa ajili ya Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii. Mfano, Wizara hiyo imeripotiwa kufanya malipo mengine ya shilingi
milioni 77 bila kufuata utaratibu wa malipo ya vocha, milioni 50 kwa wafanyakazi wanaodaiwa
kustaafu na shilingi milioni 32 kwa malipo yasiyo na umuhimu.

Imeripotiwa hivi karibuni kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitumia karibu shilingi
bilioni 1 kwa maadhimisho ya Nanenane. Ni katika mwaka huo huo wa fedha ambapo Wizarahiyo iliingia kwenye mgogoro na madaktari waliokuwa mafunzoni kwa kushindwa kuwalipa
posho ya shilingi milioni 176 tu. Hii ni takribani moja ya kumi ya fedha zilizotumika kwa
maonesho ya Nanenane. Kushindwa kupanga matumizi ya fedha kwa kuzingatia vipaumbelea
ndiko kulikosababisha mgomo wa madaktari nchini.

Fedha zilizotumiwa na Wizara ya Afya kwa sherehe za Nanenane, zingeweza kutatua matatizo
mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya kama vile kununua bandeji, mipira ya mikononi, madawa
na vifaa vingine.

Ripoti ya CAG pia inaonesha kuwa mapendekezo mengi yaliyotolewa kipindi cha nyuma
hayakufanyiwa kazi. Hii inadhihirisha ukosefu wa uwajibikaji kwa upande wa Serikali hivyo
kusababisha upotevu mkubwa wa fedha kujirudia kila mwaka. Hali hiyo inapelekea Serikali kuendelea
kuwa ombaomba na kutegemea misaada ya wafadhili.

Sikika inatoa wito kwa mamlaka husika kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na CAG na
kuwawajibisha watendaji wa Serikali waliohusika na upotevu huo. Tunapongeza kazi kubwa na nzuri
iliyofanywa na CAG kwa kuibua ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma uliofanywa na baadhi ya
watumishi wa umma na taasisi za Serikali.

Sikika imekuwa mstari wa mbele kuishinikiza Serikali kuwajibika kwa wananchi na inaitaka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa makini katika matumizi ya fedha za walipa kodi ili kuepuka
migogoro isiyo ya lazima na kuokoa maisha ya watanzania.

Bw. Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,Simu: +255 222
666355/57, Simu ya kiganjani: 0784 274039, Faksi: 2668015, barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Website: www.sikika.or.tz