Thursday, March 15, 2012

WATATU WAUAWA, WAWILI WAJERUHIWA KWA KUPIGWA NONDO MKOANI MBEYA

 

Oscar Mbalamwezi (47) mkazi wa mtaa wa Chemchemi Kata ya Igawilo jijini Mbeya aliyepigwa nondo majira ya saa saba usiku wakati akitoka kuangalia mpira juzi, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa iliyopo jijini Mbeya.
-----
WATU watatu wamefariki dunia Mkoani Mbeya katika matukio matatu tofauti, likiwemo la mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Daudi Mtereke (26), kuuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuiba baiskeli kilabuni.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 5:30 usiku huko katika Kijiji cha Nyeregete wilaya ya Mbarali mkoani hapa, ambapo marehemu alifikwa na mauti hayo baada ya kupigwa na wananchi hao, kwa kosa la kuiba baiskeli inayomilikiwa na Bwana Siwajibu Mwihula (22) mkazi wa kijiji hicho.
Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi mkoani hapa na huku upelelezi wa tukio hili unaendelea.
Tukio jingine limetokea majira ya saa 3 kamili usiku katika Kijiji cha Talatala wilaya ya Kyela ambapo Lusekelo Mwasule (40), ambaye ni mkulima na mkazi wa kijiji hicho aliuawa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali.
 Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Ipinda na upelelezi wa tukio hili unaendelea.
Aidha, majira ya saa 4 kamili usiku katika mtaa wa Chemchemi kata ya Igawilo John Ndelwa (26), ameuawa kwa kupigwa nondo kichwani na watu wasiofahamika mita chache kutoka nyumbani kwake.

Marehemu alirudi kutoka matembezi kisha alitoka ghafla na kumfungia mlango kwa nje mkewe aitwaye Lucia Ndelwa na hakurejea mpaka alipokutwa amefariki na mwili wake kugunduliwa majira ya saa 12 jioni.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana John Sanga alitoa taarifa Kituo cha Polisi ambapo walifika majira ya saa 4 kamili asubuhi na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya Rufaa iliyopo jijini Mbeya kwa ajili ya uchunguzi.

Ameongeza kuwa watu wengine wawili wamelazwa katika hospitali hiyo baada ya kupigwa nondo usiku wa kuamkia leo katika mtaa huo ambao ni Oscar Mbalamwezi (47) aliyepigwa nondo majira ya saa saba usiku wakati akitoka kuangalia mpira na mwingine jina lake halikuweza kufahamika mara moja, na wote wamelazwa wadi namba mbili.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo.


CHANZO: MBEYA YETU BLOG