Tuesday, March 13, 2012

Uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
____________

Katibu wa Bunge anatoa Taarifa kwa Umma kwamba, Uchaguzi wa wajumbe
tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia
tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.

Uchaguzi huo wa Wabunge wa  Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kwa
kuzingatia kuwa maisha ya Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka
2006, yatafikia ukomo wake  04 Juni, 2012.

Pamoja na Taarifa hii, Katibu wa Bunge ambaye ndiye Msimamizi wa
Uchaguzi huo, atatoa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa
masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni tarehe 10
Aprili, 2012, saa kumi (10.00) Jioni, na pia kuhusu siku ya uchaguzi
ambayo ni tarehe 17 Aprili, 2012 saa tano (5.00) Asubuhi, mara au
mapema baada ya Kipindi cha Maswali.

Aidha, katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti
yanayopaswa kuzingatiwa na Wagombea wa Vyama vyote vya Siasa vyenye
uwakilishi Bungeni kuhusiana na Uchaguzi huo, kwa ajili ya
kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata Wagombea kupitia Vyama hivyo,
ambao majina yao yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.

Kwa Taarifa hii, watu ambao wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa
kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wanaweza kuanza mchakato wa
kuteuliwa kuwa wagombea wa uchaguzi huo, kupitia Vyama vyao vya Siasa.


Taarifa hii imetolewa na
 Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge