Nilichojifunza kutoka mgomo wa madaktari
Nkwazi Mhango
Kanada
INGAWA mgomo wa madaktari wa nchi nzima ni tukio lililosababisha vifo ambavyo si kazi ya Mungu bali serikali, kuna somo umetoa.
Sijui kama watu wengi hasa waathirika wameliangalia kama mimi. Wenye akili wanasema kila tukio limtokealo binadamu mwenye akili ni darasa tosha. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwangu binafsi kama mwana taaluma na mkereketwa, ukiachia mbali kuwa mwanaharakati wa haki za binadamu.
Hata kama siishi Tanzania, bado nayajua masahibu na mazingira ya watu wetu. Hivyo siandiki kutokana na hasira ya kuathiriwa na mgomo wa madaktari kwa vile nilipo sina upungufu wala shida ya huduma ya madaktari, ikichukuliwa kuwa afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi (hapa si Tanzania).
Siandiki kujisifu bali kuchochea hasira na welewa wa ndugu zangu Watanzania. Sitaki nieleze hali ya afya hapa Canada ikoje kwa vile kila mtu anajua kuwa kuna mfumo mzuri kuliko hata jirani zetu kusini, yaani Marekani.
Ukimwambia Mcanada kuwa afya si haki ya binadamu anaweza kukushauri ukapimwe akili. Hayo tuyaache.
Katika mgomo uliokwisha ambao umezaa mwingine nimejifunza yafuatayo:
Kwanza, rais wetu haambiliki wala hasikii na sijui hii inasababishwa na uwezo wake wa kuelewa au anavyojiona baada ya kuwa rais.
Maana ukiangalia yule Kikwete tuliyeambiwa ni kipenzi cha watu na chaguo la Mungu unashangaa inakuwaje kipenzi cha watu na chaguo la Mungu anakuwa mkatili ambaye hajali hata taarifa kuwa kuna watu wamepoteza maisha kutokana na mgomo.
Unashangaa alipopata mshipa wa hata kuweza kwenda kwenye mkutano usio na umuhimu wala ulazima huku watu anaowaita wake wakifa kutokana na uzembe wa kawaida wa wateule wake! Kama hutajizuia kuhukumu ili usije ukahukumiwa, unaweza kumuita hata majina mengine ambayo si sahihi.
Sitaki nifikie hapo. Unashangaa ni baba au mama gani anaweza kwenda kwenye biashara wakati wale anaowaita watoto wake wakiugua na kufa kutokana na sababu anazoweza kuzuia hata kuingilia, achia mbali kuzuia.
Hivi waliopoteza maisha wangekuwa watoto wa Kikwete hata wapendwa wake kama vile Haji Mponda na Lucy Nkya, angeweza kupata hamasa kwenda Davos huku akiacha wakiteketea kwa kitu kinachohitaji si pesa wala nini, bali tamko lake? Je, huu ni ubinafsi na upogo kiasi gani?
Hakuna haja ya kupindisha maneno, rais wetu, sijui wao, hajali. Maana angekuwa rais wetu angetujali badala ya kujali kujilisha pepo kwenye vikao visivyo na ulazima ikilinganishwa na wapendwa wetu waliopoteza maisha, ukiachia mbali wale wanaouawa na polisi wake.
Siachi kujiuliza si mara moja wala mbili. Hivi hawa waliopoteza maisha wangekuwa watoto wake au hata mkewe angefanya alivyofanya? Lakini atajalije wakati yeye na familia yake wanatibiwa nje kwa pesa ya walalahoi wanaouawa na serikali kwa kuwadharau na kuwanyonya wananchi?
Nasema hivi kutokana na yaliyotokea. kwa wale waliopoteza ndugu zao serikali kwao haina maana na ni mnyonyaji wa kawaida.
Maana walipoichagua walijua itaingilia kwenye hali kama hizi. Kutofanya hivyo kunaifanya kupoteza uhalali mbele ya macho yao hata kama wanaogopa kuifurusha kutokana na woga ujinga na hata kuishi kwa matumaini.
Kitu kingine nilichojifunza ni kwamba Watanzania ni watu wa ajabu ambao hawana tofauti na kondoo kwa kushindwa kuwaunga mkono madaktari. Usishangae ukakuta wanawalaumu madaktari bila kuangalia upande wa pili ambao unatibiwa nje.
Hebu jiulize. Rais anaandamana na watu 40 kwenye ziara ya kutanua huku akiacha umma unateketea. Anapata wapi hiyo pesa ya kufanya hivyo kama si kutojali?
Cha msingi cha kuzingatia ni kwamba ni hao hao wadharauliwa na wapuuziwa wanaokatwa pesa itokanayo na kazi na jasho lao kumlipia rais na wapendwa wake kwenda kutanua wakati punda hao hao wanaomwezesha wakipukutika kama wadudu yeye asihangaike hata kutumia akili ya kawaida achia mbali elimu.
Kitu kingine nilichojifunza japo kinatia aibu ni kwamba wateule wa rais si wa kuguswa hata wakifanya madudu kiasi gani. Rejea Mponda na Nkya na wanaodaiwa kughushi vyeti vya taaluma. Yuko wapi bwana EPA bin Kagoda? Si anaendelea kutumia mahakama zetu na za kimataifa kuvuna pesa yetu huku tukijua mchezo wote na tusichukue hatua?
Rais yuko tayari kuwatoa kafara wananchi ili kuwalinda wateule wake ambao kwake ni kila kitu na si wapiga kura.
Hata hivyo ana shida gani na wapiga kura wakati hana mpango wala haki ya kugombea tena? Je, huu si utapeli wa kimfumo ukiachia mbali kuwa unyama wa ajabu ambao hata simba na fisi hawawezi kuufanya?
Kitu kingine ni kwamba Tanzania ina ombwe kubwa la uongozi kuliko ambavyo imewahi kutokea. Kiongozi wetu huyu ni ajali ya kihistoria kutokana na ukosefu wa upendo na heshima kwa wananchi, amembebesha zigo waziri mkuu kiasi cha kuonekana mbaya wakati mbaya si yeye.
Kimsingi, kinacholisumbua taifa ni ibada za sanamu, ambapo rais anaombwa badala ya kuamrishwa kama mtumishi yeyote wa umma. Nashindwa kuendelea.
Chanzo:Tanzania Daima Machi 14, 2012.