Wednesday, March 14, 2012

MKAPA AHUSISHWA NA KIFO CHA UTATA CHA MWL NYERERE.

VITA ya maneno, vijembe na kejeli kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika kampeni za
uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani
Arusha imeanza.

Baada ya juzi Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kufanya uzinduzi wa
kampeni za CCM na kuipiga vijembe CHADEMA, chama hicho jana kilijibu
mapigo kupitia kwa Mbunge wa Msoma Mjini, Vincent Nyerere, ambaye ni
Naibu Meneja wa Kampeni wa CHADEMA.

Akizungumza katika mikutano ya kampeni maeneo mbalimbali, mbunge huyo
alishusha tuhuma nzito juu ya kile alichokiita 'utata' wa kifo cha
Mwalimu Nyerere huku akihusisha na maamuzi ya Mkapa kung'ang'ania
Mwalimu aende kutibiwa Uingereza baada ya kuanza kumkosoa juu ya sera
za ubinafsishaji.

Nyerere ambaye ni mmoja wa wanafamilia wa hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere, akiwa amekulia katika familia hiyo, aliwaambia
wananchi wa maeneo hayo kuwa umefika wakati sasa Mkapa atoke hadharani
afafanue alikuwa na nia gani kumlazimisha Mwalimu Nyerere akatibiwe
Uingereza wakati mwenyewe alikuwa amekataa, akisema kuwa ugonjwa
uliokuwa unamsumbua tayari ulikuwa unajulikana na daktari wake,
Profesa David Mwakyusa, alikuwa tayari akimhudumia vizuri bila tatizo.

"Jana katika hotuba yake ametumia muda mwingi sana kuisema CHADEMA na
akanisema mimi kwa jina moja kwa moja, sasa 'kanibipu' na mimi
nimeamua kumpigia, tunamtaka kama anaweza arudi hapa Arumeru, aje
ajibu maswali ya msingi juu ya ufisadi unaomwandama. Alianza kwa kuuza
mashirika ya umma, akauza viwanda, ukienda leo miji mikubwa kama Dar
es Salaam na kwingineko, vijana wengi wamegeuka kuwa waokota makopo
kwa sababu hakuna ajira, viwanda viliuawa wakati wa Mkapa.

"Kwa kupitia sera yake ya ubinafsishaji akauza kila kitu, akauza
viwanda, wawekezaji walionunua nao wakafanya ufisadi wamegeuza viwanda
hivyo kuwa maghala ya kutunzia vitu vyao, viwanda ambavyo vingeweza
kuajiri vijana Watanzania vikauzwa kiholela kwa bei ya kutupa, vingine
wakajiuzia wao wenyewe. Misingi iliyowekwa na Mwalimu yote ikabomolewa
badala ya wao kujenga nyumba juu ya misingi hiyo.

"Mashirika yaliyokuwa yakifanya kazi vizuri au ambayo yalihitaji
usimamizi tu mzuri ili yafanye vizuri yakauzwa kiholela, yakauzwa
kifisadi, tena mkumbuke alianza kwa kuuza benki. Mwalimu kuona hivyo
akashtuka, akaanza kumhoji na kumkosoa hadharani juu ya sera yake
hiyo, jamaa (Mkapa) kuona hivyo akaona huu sasa ni usumbufu, akaanza
kumshawishi Mwalimu aende akatibiwe Uingereza, Mwalimu alikataa kabisa
akisema kuwa ugonjwa unaomsumbua tayari daktari wake anamhudumia
vema," alisema Nyerere na kuongeza:

"Mwalimu alikuwa akihoji inakuwaje reli inakufa, yeye amekazana tu na
ubinafsishaji, Mwalimu akahoji inakuwaje anatoza kodi kibao na kutunza
pesa, kumbe Mkapa tayari alikuwa anaandaa pesa za EPA ambazo baadaye
ndizo mlizisikia kupitia kashfa maarufu ya mabilioni ya EPA. Mkapa
akamng'ang'ania Mwalimua akatibiwe Uingereza, akasema naye ni mmoja wa
wanafamilia yetu, basi tukakubali, lakini mnajua kuwa Mwalimu
alikwenda anatembea akarudi amenyamaza ndani ya jeneza?

"Sasa Mkapa atuambie ukweli juu ya hili, aje ajibu maswali yote haya,
nitakuja na vigongo vingine, lazima tupambane na ufisadi hadi mwisho.
Ilifikia mahali hata taarifa za ugonjwa akawa anatoa yeye Mkapa, oooh
mara Mwalimu amepatwa na mkanda wa jeshi, mara oooh leo imekuwa hivi,
badala ya daktari wake. Baada ya Mwalimu kufariki dunia, wakamwambia
yule daktari wake agombee ubunge watampatia uwaziri, ndivyo
ilivyotokea," alisema Nyerere.

Aliongeza kusema kuwa pamoja na uhakika wa maisha yake baada ya
kustaafu ambapo anagharimiwa kila kitu kwa kodi za Watanzania, bado
Rais Mkapa alijimilikisha mgodi wa Kiwira ambao baada ya kelele nyingi
za nguvu za umma, zikiongozwa na CHADEMA bungeni na nje ya Bunge,
hatimaye umerudishwa kwa umma.

Alimtaka Rais Mkapa kujibu tuhuma juu ya ufisadi katika ununuaji wa
ndege, wakati tayari serikali ilikuwa na ndege nyingine mbili, moja
ikinunuliwa wakati wa Mwalimu na ina uhakika wa kufanya kazi kwa miaka
100 iwapo ingefanyiwa matengenezo kadiri inavyotakiwa.

Pia akamtaka kujibu hoja za Watanzania juu ya ufisadi wa rada, ambao
hata Waingereza wanaupigia kelele, baada ya yeye na wenzake serikalini
kufanya 'dili' kujinufaisha wao badala ya kuongoza wananchi.

Nyerere aliongeza tuhuma kwa Mkapa akisema kuwa pia anatakiwa kujibu
hoja juu ya mauaji ya Zanzibar ya mwaka 2001, ambapo kwa mara ya
kwanza Tanzania mbali ya serikali kuua raia wake kwa risasi,
ilizalisha wakimbizi kwenda nchi za Kenya na Somalia.

Akifafanua tuhuma za ufisadi dhidi ya Rais Mkapa, mbunge huyo alisema
kuwa kama Mkapa anataka kueleweka mbele ya Watanzania wenye uchungu na
nchi yao, anatakiwa kujibu hoja za msingi juu ya tuhuma hizo za
ufisadi zinazomwandama tangu akiwa madarakani hadi anastaafu.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akihutubia mamia ya wakazi wa maeneo ya
Lenguruki, Poli, Sing'isia na Nkoaranga, alisema kuwa rais huyo
mstaafu anapaswa kuwa mmoja wa watu wa mwisho kusimama mbele za watu
kwani hali inayolikabili taifa kwa sasa, ikiwamo ufisadi uliotapakaa
ndani ya chama chake na serikali ya CCM, iliasisiwa tangu wakati wa
utawala wake, kwa kuanzia na sera za ubinafsishaji zilizoua misingi ya
viwanda iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake, mgombea wa CHADEMA Joshua Nassari, alisema kuwa
amegombea kwa nia ya kubeba 'mizigo' ya wana wa Arumeru kwani
anaitambua, hivyo yuko tayari kuibeba kwenda nayo bungeni Dodoma na
katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, kuwasemea na kuiwajibisha
serikali ili iwajibike kwa wananchi.

Joshua alionekana kuwagusa wananchi wa maeneo hayo pale alipokuwa
akizungumzia kero za kila eneo husika, kama vile ardhi, maji, afya na
elimu na namna ambavyo wanaweza kushirikiana pamoja na mbunge wao
katika kuyatatua, iwapo watamchagua yeye ambaye amezaliwa na kukulia
katika maeneo hayo na yuko tayari kuwatumikia akiwa anaishi katika
maeneo ambayo wanaishi wao pia.

Aliwataka watu wa Meru wasidanganyike na maneno ya Mkapa kuwa
atakwenda kumshauri Rais Jakaya Kikwete ashughulikie matatizo ya ardhi
katika wilaya hiyo, kwani alishindwa kufanya hivyo wakati akiwa na
mamlaka ya urais, hawezi kuifanya kazi hiyo kwa sasa kwani rais ana
hiari ya kukubali au kukataa ushauri wa mtu yeyote kwa mujibu wa
katiba yetu mbovu.

"Kwa mujibu wa katiba yetu mbovu ambayo tunataka tuiandike upya, rais
halazimiki kuchukua ushauri wa mtu yeyote, hivyo Kikwete anaweza
kukataa ushauri wake huyo Mkapa, aje ajibu hoja hapa kwa nini
alishindwa kutatua matatizo ya ardhi kwa watu wa Arumeru wakati akiwa
madarakani?" alihoji Nyerere.

CHANZO: Tanzaniadaima 14 Machi 2012