Tuesday, March 20, 2012

AL QAEDA NA AL SHABAB WAKO KIBAHA.

UONGOZI wa Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyoko kata ya Mwanalugali,
wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, umewasimamisha masomo wanafunzi 32 kwa
tuhuma za kuhusika kuunda makundi ya Al-shaba na Al-queda na kufanya
vurugu hivi karibuni.

Wanafunzi hao wamesimamishwa baada ya kikao cha uongozi wa shule na
wazazi wao hadi hapo bodi hiyo itakapokaa na kufanya maamuzi ya
mwisho.

Akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo, Mwalimu wa Taaluma,
Nuru Manfred, alieleza kuwa wanafunzi hao wameishushia hadhi shule
hiyo, hivyo hawana budi kusimamishwa na taratibu nyingine kufuatwa.

Aliongeza kuwa wanafunzi hao ambao waliunda makundi hayo mawili ni wa
kidato cha pili na cha tatu.

Mwalimu Manfred, alisema kuwa sambamba na hilo, pia mwanafunzi wa
kidato cha pili, aliyemtaja kwa jina moja la Mbaraka, amesimamishwa
masomo kutokana na tuhuma za kuishi na mwanamke kinyumba.

Naye mkuu wa shule hiyo, Aron Ndunguru, alisema kuwa uongozi wa shule
hauna uwezo wa kuwafukuza wanafunzi hao bali bodi ya shule pekee ndiyo
inaweza kufanya hivyo na kwamba kwa sasa wanasubiri kikao cha bodi
ambacho kitafanya maamuzi ya mwisho.

Chanzo: Tanzaniadaima