Monday, January 30, 2012

Twiga yaifanyia mauaji Namibia

Baadhi ya wachejazi wa Twiga Stars wakishangilia ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Namibia jana.
Lucy Mgina na Khadija Mngwai
WACHEZAJI wa Twiga Stars, Mwanahamisi Omary na Asha Rashid ‘Mwalala’ jana waliogelea fedha kwa kutunzwa na mashabiki wakati wakitoka uwanjani, baada ya kuiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Namibia katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.

Baadhi ya mashabiki waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa kuangalia pambano hilo, walikuwa wakitoa noti za kuanzia shilingi 500 hadi 10,000 kwa wachezaji hao hatari ambao walifunga mabao mawili kila mmoja huku lingine likifungwa na Etoe Mlenzi.Mbali na fedha hizo za mashabiki, timu nzima ya Twiga Stars jana ilikabidhiwa shilingi milioni nne kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni na michezo, Dk Emmanuel Nchimbi pamoja na wabunge walioahidi kutoa shilingi milioni moja ikiwa timu hiyo itashinda.
Katika mchezo huo, mabao ya  Namibia yalifungwa na Juliana Skrywer, pamoja na bao moja la zawadi baada ya beki Fatma Bashir kujifunga.

Twiga walionekana kutawala sana mchezo huo. Licha ya Namibia kusawazisha mabao mawili ya kwanza, lakini walipoteana katika dakika za mwisho na kuwapa mwanya kinadada wa Kitanzania kuonyesha makeke yao na kufanikiwa kupata mabao matatu katika dakika 10 za mwisho.Baada ya mechi hiyo, Twiga walipata wakati mgumu walipotaka kuondoka uwanjani baada ya mashabiki kulizingira gari lao huku wakishangilia na kuimba kwa furaha, polisi waliingilia na kutoa msaada. Baada ya ushindi huo, Twiga itacheza na Misri au Ethiopia katika hatua inayofuata na kocha wa timu hiyo, Boniface Mkwasa, ametamba kuendeleza ushindi.

Source: GlobalPublishers.