Sunday, January 15, 2012

My Tribute to my friend the Late Regia Mtema!




Kamanda Umechanua na kunyauka.Pumzika kwa amani!

 

"Tuache masihara, hakikisha unaninunulia ukiwa unarudi vitabu hivi; Balance Scorecard na Iron Lady cha Margeth Thatcher maana nimesikia upo nje ya bongo" aliniambia Regia, name nikamjibu "sawa. usijali nitakununulia"! Sikufahamu kuwa ndiyo yalikuwa mawasiliano yetu ya mwisho kati yangu na rafiki yangu Regia tuliyofanya tarehe 12.01.2012 na hata wala hatutoonana name kupata fursa ya kumpatia vitabu kama ombi lake.

 

Kwangu ni kama ndoto. Ukishtuka isiwe kweli. Lakini si njozi. Tayari Regia amefunga kitabu cha maisha yake duniani angali katika umri moto wa ujana.

 

Angali akiwa bado na mipango na mikakati mwingi kutelekeleza.

 

Alikuwa rafiki yangu ambaye tulishazoea sana kiasi cha kutaniana na kuongea upuuzi upuuzi mwingi sana……maana hata binadamu wa namna gani kuna watu wake ambao anataniana nao na hata kuongea upuuzi upuuzi.

 

Niandikapo tanzia hii kwa laptop nayo ni sehemu yenye kuongeza machungu na simanzi. Kwani nakumbuka aliniomba nimsaidie kupata laptop kwa kazi zake, nami nilikuwa nataka kubadili kompyuta. Hivyo nikamwakikishia nitaenda kumchagulia kompyuta nzuri ambayo ataipenda maana alishachoka kuzunguka madukani bila mafanikio hadi akafikiria kuagiza nje. Nilikwenda naye, na kumwonyesha kompyuta ambayo alipenda hivyo tukanunua pamoja aina moja ya kompyuta.

 

Alikuwa mtu ambaye nilikuwa nimeshibana sana na nilifurahishwa sana nae mara kwa mara tulipokuwa tukikutana. Tulisoma pamoja kozi ya mwaka mzima ya uongozi ambayo ilizidi kutuweka karibu zaidi na zaidi. Mengi tukifundishana na kuelekezana. Kozi tuliyoifanya mwaka 2006/2007.

 

Nakumbuka ni kipindi hicho na kuendelea ndipo alikuwa mstari wa mbele katika kazi za kisiasa kupitia chama cha Chadema. Mara kwa mara nilikuwa namwambia kuwa angalikuwa mbunge baada ya uchaguzi wa mwaka 2010. Jambo ambalo mara nyingi alikuwa akikwepa kulijadili kwa kina na kuyeyusha kwa mizaha na pale nikimsisitiza kuwa sikuwa katika mizaha aliishia kuniambia siasa ni safari ndefu lolote linaweza kutokea hivyo tudumu katika kuombeana na utashi wangu mwema utimie.

 

Ifahamike, wakati namwambia hayo juu ya uwezekano wake kuwa mbunge hakuwahi kuniambia juu ya kufikiria kusimama kugombea, na wala hakuwa ameniambia juu ya jimbo la Kilombero.

 

Nilishawishika na uwezo, dhamira, jitihada alizokuwa nazo na hakika kwa yeye kuwa katika siasa na kufanya kazi za chama kwa kujitolea na kujituma niliona ni miongoni mwa vigezo muhimu sana ambavyo vilimpatia zaidi na zaidi uwezo na ufahamu wa kisiasa hivyo nilitaraji yeye kugombea na kushinda mwaka 2010. Maneno yangu kwake daima yalikuwa msukumu kumuonyesha kuwa anaweza na kama alikuwa akisita kuthubutu apate ujasiri wa kusonga mbele.

 

Na mwaka 2010, ndipo aliniambia dhamira yake ya kuingia moja kwa moja katika siasa. Kusimama katika jimbo na kushindana. Taarifa hiyo kwangu ilikuwa furaha kuu. Nilimwamini, na kuwa na uhakika angalifanya vizuri na kuibuka kidedea.

 

Ukiwa mwaka wa mikiki mikiki mingi kisiasa, licha ya majukumu mengi, alidumu kuwasiliana nami na kubadilishana mawazo hapa na pale. Na hatimaye hata dakika za mwisho za kusubiri matokeo nilikuwa na furaha sana kuona amemudu kufanya vyema. Licha ya kutotangazwa mshindi. Hakika Regia alikuwa mwakilishi imara wa wanakilombero.

 

Nilifurahi zaidi nilipoona orodha ya wabunge rasmi wa Chadema kupitia viti maalumu jina lake likiwamo, nakumbuka nilikutana nae na kwa furaha niliishia kumwambia; "unakumbuka lakini nilikwambia utakuwa mbunge?!" yeye hakujibu neno bali kicheko tu na kunirushia matani ya hapa na pale.

 

Uwakilishi wa kibunge aliutumikia vyema pasi kuchoka, akijituma licha ya changamoto nyingi zilizopo katika uendeshaji wa siasa zetu nchini. Hakukata tamaa na kurudi nyuma. Hakuacha kujifunza, hakuacha kuwa msikivu!

 

Ni mapambano haya ya kuleta mabadiliko katika jimbo la Kilombero ndiyo pia yalimsukuma Regia kuja na wazo la kuwa na vuguvugu "movement" ya maendeleo ndani ya Kilombero. Katika mwaka wa kiuchaguzi alikuwa tayari akitumia kauli ya; "Kilombero for Change" (Kilombero kwa Mabadiliko). Nakumbuka tulikutana na kujadiliana juu ya umuhimu wa kupiga hatua ya kutoka kuwa "movement" na chombo rasmi, kuwa taasisi kwa jina la Kilombero for Change. Jambo ambalo baada ya siku kadhaa aliniomba nilisimamie mwanzo mpaka mwisho kuhakikisha chombo kinasajiliwa na kuanza kujiendesha. Kazi ambayo niliipokea na kuitenda kwa uaminifu mkubwa nikijua nasaidia mabadiliko kwa wanakilombero na zaidi namsaidia rafiki yangu katika kutekeleza ndoto aliyonayo.

 

Ingawa bado shirika halikufikia hatua ya kusajiliwa, lakini tulimudu kukamilisha taratibu zote zilizostahili katika usajili kama Katiba, nembo, jina na vingine vingi tuliweza kuvikamilisha nikisaidiwa na marafiki wa karibu katika harakati. Tukiwa tunasubiri jambo moja tu, orodha ya majina ya watu ambao aliwaamini walikuwa imara kuanza kutenda kazi katika ngazi ya wajumbe wa bodi. Mara kwa mara nikiwa namkumbusha juu ya kukamilisha mchakato wa kuanzisha taasisi, alikuwa msikivu na kunikumbusha pia umuhimu wa kuhakikisha anapata watu wazuri katika bodi na si bora watu tu kutimiza hitaji la uanzishwaji wa taasisi.

 

Licha ya majukumu mazito ya kibunge, daima alikuwa mwepesi katika mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii na hata simu yake. Alikuwa mshirika imara na mwepesi kushughulikia jambo hasa upatikanaji wa taarifa au nyaraka kwa wakati. Nilimtegemea sana kwa hili na yeye hakuniangusha daima.

 

Kwangu daima aliendelea kuwa rafiki wa karibu zaidi hata ya nyadhifa yake!

 

Najaribu kutafakari maneno ya Jim Reeves katika wimbo wake wa; "This world is not my home"! Siamini maneno haya sasa yanarindima kwa rafiki yangu Regia.

 

Licha ya majonzi nafarijika sana kwa Regia kumudu kufanya mengi katika umri wake mbichi wa ujana.

 

Amemudu hata kuthubutu kuingia katika siasa tena kupitia upinzani na zaidi kugombea kiti cha ubunge kupitia jimbo! Wengi sana wamekuwa wakiahirisha uamuzi na kusubiri miaka ipite kwanza. Wengi kwa kuwa wanawake wamekuwa wakirudi nyuma na kuacha kugombea kupitia majimboni. Amemudu kuishi na kuitumikia nchi, si tu  katika harakati kupitia mashirikia ya watu wenye ulemavu bali katika kutunga sheria na kuisimamia serikali. Amejitahidi kurejesha matumaini na fikra mbadala kwa wanakilombero, kwa vijana,  kwa wanawake na zaidi kwa watu wenye ulemavu. Amedhihirisha inawezekana!

 

Licha ya nafsi zetu binadamu kutokumudu kuhimili majonzi na simanzi zito na kuishia kuanguka katika kilio, naamini Regia huhitaji machozi yetu sana sasa kama unavyohitaji sala zetu. Daima nitakuweka katika sala zangu. Daima tumuweke katika sala zetu!

 

Pole sana kwa Remija natambua uchungu ulio nao kwa kupoteza pacha mwenzako. Pole sana baba na mama, najua mpo katika simanzi na majonzi makuu ya kumpoteza kijana wenu. Ni uchungu gani kumlaza kijana mbichi kama Regia!Mungu awape faraja na moyo wa saburi. Pole kwa familia nzima ya Regia, ndugu, jamaa na marafiki. Naamini ni kipindi kigumu sana, tuweka tumaini letu kwa MUNGU.

 

Makamanda wote wa CHADEMA poleni sana. Kwa namna ya kipekee John Mnyika (MB) ambaye amekuwa  chachu, taa na muongozo mkubwa kisiasa kwa Regia,pole sana. Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu Dr.Slaa, Makamu Katibu Mkuu Zitto na viongozi  wengine wote pamoja na maafisa na watendaji wa chama Makao Makuu poleni sana. Kamanda alisimama kidete, alipambana, hivyo daima tunu kubwa itakuwa kuendeleza mapambano; Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke!

 

Poleni sana wananchi wa jimbo la Kilombero!

 

Poleni sana wabunge na bunge zima kwa ujumla!

 

Zaidi poleni sana wananchi wote wa Tanzania.

 

"Even though crying is a human act that helps in healing our pains in our souls…now Regia needs much our prayers than tears"!! (Hata kama kulia nikitendo cha kibinadamu kinachosaidia kutuliza maumivu katika roho…sasa Regia anahitaji zaidi sala zetu zaidi ya machozi!)

 

Kwa kheri Kamanda! Ulale mahala pema peponi.

 

© Michael Dalali, 14.01.2012