Saturday, January 21, 2012

BASI LA NEW FORCE LAUA STENDI YA MABASI MBEYA

ABIRIA aliyefahamika kwa jina moja la Amina mkazi wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya alikufa papo hapo katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani kutokea Mbeya baada  ya basi la New Force kuparamia ukuta wa mgahawa uliopo mkabala na Ofisi za Mabasi ya Kampuni hilo.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 5:00 usiku wa Ijumaa ya Januari 20 mwaka huu  katika Kituo hicho cha Mabasi yakitokea mikoa mingine.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kondakta wa basi hilo aliyejulikana kwa jina la Januari Kapinga aliingia ndani ya basi hilo lenye namba za usajili T 853 AVQ aina ya Yutong lililokuwa likitokea Dar es Salaam baada ya abiria wote kushuka ndipo alipolikurupua kwa nguvu na kumshinda hatimaye kuparamia ukuta.
Abiria aliyefariki alikuwa safarini kuelekea masomoni mkoani Tabora na wakati gari likiparamia ukuta wa mgahawa huo alikuwa akipata chakula cha jioni
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema licha ya mmoja huyo kupoteza maisha, lakini watano wamejeruhiwa.
Aidha kondakta wa basi hilo alitoroka na kwenda kusikojulikana na juhudi za Jeshi la Polis kumtafuta zinaendelea na hadi sasa dereva wa basi hilo anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.
Kwa upande wake Noah Mwakatumbula Mwenyekiti wa Kituo cha Mabasi mkoani Mbeya yaendayo mikoani amewataka madereva waliopewa dhamana ya kuendesha vyombo hivyo na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waache mara moja tabia ya kuacha funguo za vyombo vyao vya usafiri.
Imeandikwa na Ezekiel Kamanga na Jabir Johnson Januari 21, 2012
Kutoka: JAIZMELA LEO