Ndugu zangu,
Kuna tuliomsoma mwanafasihi Shaaban Robert. Kuna mahali kwenye kitabu chake ' Nchi Ya Kusadikika' Shabaan Robert anamwelezea mchwa anayekaribia kufa.
Kwamba huota mbawa. Hukiacha kichuguu . Yumkini ataruka juu sana. Atakwenda mbali. Lakini, huko angani hufika mahali, mbawa hupukutika. Mchwa ataanguka chini. Mbali na kichuguu.
Hapo, mchwa hukabiriwa na hatari kubwa. Hawezi kuruka tena, na yu mbali na kichuguu. Na kichuguu ni taasisi. Hivyo, mchwa anaweza kuliwa na kinyonga, au hata chura. Na akinusurika na wawili hao, aweza kukanyagwa na unyayo wa mwanadamu, au hata tairi la baiskeli. Mchwa atakufa.
Naam, mengine tuyafanyayo hupelekea maanguko yetu. Hata kama mwanzoni huonekana kutupaisha juu angani.
" Nafikiri, ndio maana naishi"- Anasema mwanafalsafa Rene Descartes.
Na maarifa ya Sayansi yanatusaidia kuyabaini mahusiano kati ya dunia tunayoishi na mazingira yanayotuzunguka. Hiyo ni falsafa ya kivitendo. Ndio iliyo bora kuliko ile dhanifu- Speculative.
Iweje basi tumekuwa ni watu wa kuishi kwa dhania na hata kusambaza uvumi?
Ngoja nijiandae kwa safari yangu ya Iringa kesho alfajiri.
Usiku mwema.
Maggid
Msamvu, Morogoro.
http://mjengwa.blogspot.com
http://mjengwa.blogspot.com