Zitto bado amchachafya Spika, ni kuhusu posho Bungeni |
Sunday, 12 June 2011 21:27 |
Neville Meena, Dodoma HOJA inayoshinikiza kufutwa kwa posho za wabunge pamoja na watumishi wengine wa umma imeendelea kuzua majibizano baina Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe na Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda. Wakati Ofisi ya Spika wa Bunge inasisitiza kwamba fedha za posho za vikao zitawekwa katika akaunti ya Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema) hata kama hazitaki, Zitto amesema kwamba sasa hatasaini karatasi ya mahudhurio. Zitto alisema jana mjini hapa kuwa tangu Juni 10, mwaka huu alishamjibu Spika akikataa "kushinizwa kuchukua posho za vikao" (sitting allowances) akisisitiza kwamba hatua atakayoichukua ni kutosaini karatasi za mahudhurio katika vikao vyote. Mahudhurio hayo ndiyo hulalalisha mbunge kupewa posho hizo. "Kuanzia kikao cha juzi cha Tume ya Mipango, sikusaini na mkitaka nendeni mkaangalie ile orodha na kesho ndani ya Bunge sitasaini ili kuondoa uhalali wa kupewa posho hizo, sasa hapo tutaona watanilazimisha kwa njia gani," alisema Zitto. Juni 10 mwaka huu, Bunge lilimwandikia Zitto barua likimweleza kuwa ofisi yake haiko tayari kupeleka posho zake katika Taasisi ya Kigoma Development Inititive (KDI), kama alivyoomba na kwamba fedha hizo za posho zitaendelea kuwekwa katika akaunti yake benki. "Nimeelekezwa na Spika nikufahamishe kuwa, pamoja na nia yako nzuri uliyoionyesha, utaratibu wa Ofisi ya Bunge kwa sasa ni kulipa stahili za wabunge moja kwa moja kwa wabunge husika kwa mujibu wa sheria...," imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Nenelwa Mwihambi Wankanga kwa niaba ya Katibu wa Bunge na kuongeza: "Isipokuwa mara baada ya kupokea stahili zako wewe mwenyewe unaweza kuamua uzipeleke wapi." Barua hiyo ilikuwa ikijibu ya Zitto aliyoiandika Juni 7, mwaka huu kwa Katibu wa Bunge akikaataa posho zake za vikao na kutoa maelekezo kwamba iwapo ni lazima alipwe basi fedha hizo zielekezwe KDI kuanzia Juni 8, mwaka huu.Lakini Juni 10, Zitto alijibu barua ya hiyo akikataa kile alichokiita: "Shinikizo la kupokea posho za vikao" kwa kusema asilipwe fedha hizo kuanzia Juni 8. "Kwa kuwa umesema kwamba sheria inawataka kulipa stahili za wabunge moja kwa moja (ingawa hukutaja ni sheria ipi) na kwamba ni kama ofisi yako inanilazimisha mimi kupokea stahili ambayo ninaamini sistahili. Nakupa taarifa kwamba nimeonelea bora kukataa stahili hii," inasema sehemu ya barua ya Zitto kwenda kwa Spika na kuongeza: "Hivyo ninaelekeza kwamba ofisi yako isinilipe stahili ya posho ya kikao (sitting allowance) kuanzia Juni 8, 2011". Gazeti hili lilipomuuliza Zitto ni kwa jinsi gani atakavyokataa fedha hizo alisema: "This is very simple (ni rahisi sana) kwani hata juzi kwenye ile semina ya mipango sikujiandikisha na kuanzia kesho nikiingia bungeni sitajiandikisha, hapo watanipata vipi?" Kwa mujibu wa Zitto, posho za vikao hutolewa kwa kuzingatia mahudhurio bungeni na kwamba wabunge wasiosaini kwenye fomu hizo, huwa hawapewi posho hizo.Alisema kutoka na msingi huo, hakutakuwa tena na ugomvi baina yake na Spika wa kulazimishwa posho za vikao, kwani hawezi kulipwa fedha hizo kama asiposaini karatasi za mahudhurio hatua ambayo tayari ameanza kuitekeleza. Msimamo wa CCM Wakati Chadema wakiendelea kulumbana na Serikali kuhusu pendekezo la kufutwa kwa posho za wabunge pamoja na zile za watumishi wengine wa umma, CCM kimesema suala hilo linajadilika na kwamba si busara kupinga kila kinachotoka upande wa pili. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM), Nape Nnauye alisema mjini Dodoma juzi kuwa chama hicho hakipingi wala kuunga mkono kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa umma, lakini akabainisha kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa na kufikiwa mwafaka baina ya pande zinazopingana. Alisema malumbano yanayoendelea nje ya Bunge baina ya pande zinazopingana hayana tija na kwamba wabunge wote wa CCM na wapinzani watumie fursa walizonazo katika vikao kufikia mwafaka wa suala hilo."Kama posho za vikao zipo kisheria au kisera, mifumo ya kufanya mabadiliko iko wazi na inajulikana, sasa malumbano yanayoendelea nje ya vikao vya bunge sijui ni kwa faida ya nani?" alisema Nape na kuongeza: "Kwa mfano, mimi nafahamu Zitto kwamba ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge, angeweza kuanzia huko, lakini kwa kuwa ameishatamka hadharani si lazima wale wanaojibu nao wazungumze hadharani, wanaweza kuliingiza katika taratibu za kawaida za vikao na kujadili kisha kukubaliana." Kauli hiyo ya Nape ambaye ni msemaji mkuu wa CCM, huenda isiwafurahishe wabunge wengi wa chama hicho ambao kwa nyakati tofauti wamesikika na kunukuliwa wakibeza msimamo wa Chadema kuhusu posho za vikao kwamba haziwezi kuondolewa na kwamba Chadema wanatafuta umaarufu usio na msingi. Malipo ya Posho Habari kutoka katika vyanzo mbalimbali zinasema kwamba malipo ya posho kwa watumishi wengi wa umma yamekuwa yakifanywa kiholela kiasi kwamba baadhi ya maofisa wengine serikalini wamekuwa wakipata posho zaidi ya moja katika tukio moja. Habari kutoka serikalini zinasema kufutwa kwa posho za vikao kutaongeza tija kwani ni kweli kwamba watumishi wa umma hasa wale wa ngazi za juu wamekuwa wakiendesha vikao kila siku kwa lengo la kujikusanyia posho, hata pale vikao hivyo vinapofanyika katika ofisi za taasisi husika. Mmoja wa watumishi wa taasisi moja ya elimu ya juu nchini ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema mjini Dodoma kuwa: "Pale kwetu mbona ndiyo mchezo, tena wakati mwingine utakuta idara inasimamia mambo matatu, lakini kila jambo linaandaliwa kikao chake na kila kikao kina posho yake, wasipofanya hivyo watakula wapi?" Mtumishi mwingine katika moja ya wilaya zilizoko Kusini Magharibi ambaye pia yupo mjini hapa alisema katika halmashauri anayofanyia kazi, watendaji wakuu hulipwa posho za kujikimu (per diem) hata kama wasipolala nje ya kituo cha kazi."Unaweza kusikia kachukua posho ya siku 10 kwenda huko vijijini lakini baada ya siku mbili unamkuta karudi ofisini kwa madai kwamba kuna dharura na ndiyo safari imeisha wala haendi tena na pesa harudishi," alisema na kuongeza; "Sasa bwana ninyi waandishi mtusaidie kufichua haya maana sisi wadogo ndiyo tunaonyayasika, ukienda kudai hata hela yako halali hupati, unazungushwa hata wiki mbili lakini hawa wakubwa wanachota tu." |