Friday, October 15, 2010

Ndoto za Nyerere zimewekwa kando

Thursday, 14 October 2010 08:30

Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
WASOMI, wanasiasa na viongozi wa dini wamesema ndoto za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere zimemezwa na watu wachache wenye uchu wa madaraka na wasiojali wala kuitakia mema Tanzania.

Wakitoa maoni yao jana kwa nyakati kuhusiana na maadhimisho ya miaka 11 tangu Mwalimu Nyerere alipofariki dunia inayofanyika leo, wanazuoni na viongozi hao waliwataka Watanzania mwaka huu kumwenzi muasisi huyo taifa kwa kutowachagua watu wabaya na kuwahimiza wagombea wa nafasi mbalimbali kuheshimu matokeo ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Okotba 31.

Walisema maadili ya uongozi yaliyoachwa na Nyerere yamesahauliwa na viongozo hivyo kuna haja kwa taifa kurejesha maadili hayo ili kuinusuru nchi.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya damu Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alikoenda kutibiwa.


''Moja ya mambo ya msingi ambayo tunapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere, ni kuheshimu maamuzi ya wananchi katika kuchagua mgombea wa urais, ubunge na udiwani. Kuchakachua matokeo, itakuwa ni jambo la hatari,'' alisema aliyewahi kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Arcado Ntagazwa.

Ntagazwa alisema kuheshimu maamuzi ya wananchi ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

Aliwataka wagombea watakaoshindwa katika uchaguzi huo ikiwamo  rais anayetetea nafasi yake Jakaya Kikwete kukubali matokeo na kuachia madaraka kwa amani kama atashindwa.

''Kitu muhimu, hata kama rais aliyepo madarakani anataka kurudi madarakani, akishindwa katika uchaguzi akubali kuachia madaraka kwa kuwa hiyo ndiyo demokrasia,'' alisema Ntagazwa.

Ntagazwa ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Muhambwe kwa  tiketi ya Chadema, alisema viongozi wengi barani Afrika ikiwamo Tanzania, wanakataa kuachia madaraka kwa hiari yao kwa kuogopa mabaya waliyoyafanya wakiwa madarakani.

Akimzungumzia Nyerere, Ntagazwa alisema viongozi nchini hawezi kumuenzi kwa vitendo kutokana na kutokuwa safi kama alivyokuwa yeye.

''Matendo yetu machafu sisi viongozi ndiyo yanayotufanya tushindwe kumuenzi Nyerere,'' alisema Ntagazwa ambaye alitoka CCM na kuhamia Chadema Agosti 7, mwaka huu.


Alibainisha kuwa  Nyerere aliachia madaraka kwa hiari yake, tofauti na viongozi wengi ambao wanaamini hilo sio sahihi.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Leonard Mtaita alisema: "Nataka niseme neno moja, nalo ni hili, yamekuwepo maneno mengi ya kumuenzi Nyerere bila matendo. Ukweli ni kwamba, maadili aliyoacha Nyerere yameliwa na mchwa na kuisha kabisa".

Mtaita alisema inasikitisha kuona maadili hayo yaliyoanzishwa na Nyerere kupitia Azimio la Arusha yamekwisha na matokeo yake watu hawaridhiki na viongozi hawaridhiki.

Kwa mujibu wa Mtaita, hali ya uongozi ni mbaya hasa ndani ya chama tawala CCM na kwamba, Nyerere angekuwepo leo, angeshangaa jinsi chama kinavyokumbatia undugu, ukabila na urafiki.

"Nyerere angekuwepo leo, angeshangaa jinsi mambo yalivyo ndani ya CCM. Inasikitisha. Ndani ya CCM kuna undugu, ukabila au urafiki. Tusingetegemea aliyeshinda kwa kuchaguliwa na wananchi kuenguliwa kwa maslahi ya viongozi. Hii inashusha hadhi ya chama," alisema Mtatita.

Aliongeza: "Mimi ni mwana CCM niliipenda kutokana na Mwalimu Nyerere na nina kadi ya CCM siwezi kuficha. Lakini, hali hiyo ilinishtua. Mizengwe ni hatari ndani ya chama. Nasema wakati umefika sasa maadili ya Azimio la Arusha yarejeshwe".

Alifafanua kuwa kuna tofauti kubwa kati ya  CCM aliyoiacha Nyerere na ya sasa ambayo alisema hivi sasa viongozi wanakiongoza chama kwa misingi ya matabaka ya undugu, ukabila na urafiki kutoka na kurithishana madaraka.

Mhadhiri wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Gilliard Wilson alisema Tanzania ya leo haina mikakati ya kumuenzi Baba wa Taifa na imeamua kupuuza.

“Katika uchaguzi tunaona fedha nyingi zinatumika. Mwalimu alisema tukiona watu wanatumia fedha nyingi katika uchaguzi tuwaulize wanazitoa wapi? Kama wamekopa wamezikopa kwa nani na watazilipa vipi?”alisema Wilson.

Aliongeza: “Wasomi wengi tumeweka elimu kando na kushabikia ufisadi. Hii inatokea pale tunapojifanya tunafanya tafiti na kusema fulani maarufu au uchumi wa nchi umekua, wakati bado kuna mfumuko mkubwa wa bei katika bidhaa mbalimbali.”

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Simoni Lushakuzi alisema: “Tofauti kati ya Serikali ya Nyerere na serikali za sasa ni vipaumbele. serikali sasa haina fedha wakati serikali ya Nyerere ilikuwa nazo," alisema.

Lushakakuzi aliongezea kuwa Nyerere alianzisha Chuo cha Usafirishaji, Chuo cha wataalam wa maji na vyuo vya kilimo ambavyo baadhi yake vimekufa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii, Chuo Kikuu cha Tumaini, Egidio Chaula alisema Watanzania wanapaswa kumuenzi Nyerere kwa uzalendo aliokuwa nao kwa maslahi ya Tanzania na wananchi wake.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mliamani, walisema wanasikitishwa na viongozi wa sasa kwa kujilimbikizia mali.

Matilda Sabayi anayesoma Shahada ya Udaktari wa falsafa ya Jiografia alisema wananchi wanamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa mambo mengi, kubwa likiwa ujamaa ambao sasa haupo.
Mwanafunzi mwingine wa shahada ya uchumi, Elham Aziz alisema mfumo wa kupata uongozi enzi za Mwalimu Nyerere ni tofauti na sasa ambapo watu wanapata madaraka kwa kutumia rushwa, kujuana na urafiki.

Imeandaliwa na Exuper Kachenje, Sadick Mtulya, Petro Tumaini, Aziza Masoud na Beatrice John 
(Source Mwananchi)