Thursday, October 07, 2010

Mgombea Ubunge anaswa makaburini......

Na Mwandishi Wetu - GPL

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, imani za kishirikina zimeanza kuamka, mkoani Mwanza mmoja wa wagombea ubunge amenaswa usiku wa manane makaburini.
Habari zisizo na shaka zinafunuliwa kuwa mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye jina na jimbo lake vinahifadhiwa kwa sasa, alinaswa wikiendi iliyopita.
Chanzo chetu makini kilipasha kuwa mgombea huyo, alifika kwenye makaburi (hatuyataji) majira ya saa 7:24 usiku na kuliendea kaburi mojawapo kisha kusimama juu yake.
Ilielezwa kuwa mgombea huyo akiwa na wapambe wake wawili, walifika makaburini hapo wakiwa wanatumia gari aina ya Crester G100 Metallic.
“Alishuka na mpambe mmoja ambaye alibeba jagi la maji na yule mwenzake aliyekuwa dereva alibaki. Waliongozana mpaka juu ya kaburi, mgombea akapanda juu ya kaburi, akavua nguo, halafu yule mwingine akammiminia kimiminika ambacho kilikuwemo kwenye jagi,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zinaendelea kupasha kuwa baada ya mgombea ubunge huyo ‘kuoga’ kile kimiminika, alipiga goti juu ya kaburi lile na kuinamisha kichwa kama ishara ya kufanya maombi kwa zaidi ya dakika 20.
“Baada ya hapo alisimama tena juu ya kaburi na kuoga kimiminika kilichokuwa kimebaki kwenye jagi, halafu alivaa nguo na kurejea kwenye gari,” alisema mtoa habari wetu.
Chanzo chetu ambacho kinatoka kinatoka kambi ya upinzani na mgombea huyo, kilisema kuwa awali alipata habari kwamba mgombea huyo atazuru makaburi hayo kwa lengo la kung’arisha nyota ya ushindi kama ambavyo amepewa masharti na mganga wake.
Kilisema, baada ya kupata taarifa hizo, walifunga safari mapema makaburi hapo kabla ya saa mbili baadaye kumshuhudia mgombea huyo akiwasili na wapambe wake.
Gazeti hili baada ya kuzinasa hizo, lilimuendea hewani mgombea ubunge huyo ambaye baada ya kusomewa tuhuma zake, alijing’ata ulimi kwa kutoa maelezo yasiyo na ufafanuzi: “Unasema kuna watu waliniona? Aah, hiyo siyo sawa kabisa na kwanini watu wananifuatilia kiasi hicho?” Baada ya hapo alikata simu