Kada wa CCM aipa tena Chadema Sh100 milioni |
Saturday, 23 October 2010 08:32 |
Source :Mwananchi. Fidelis Butahe na Hussein Issa CHADEMA imeongezewa nguvu tena katika wiki ya mwisho ya kampeni baada ya kada wa CCM, Mustafa Sabodo kuichangia tena Sh100 milioni, huku akidai kuwa chama hicho tawala kimepoteza mwelekeo wa kisiasa. Sabodo, ambaye ni mfanyabiashara maarufu, alitoa tena kiasi kama hicho cha fedha Julai 12 mwaka huu kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi na kuahidi kuwa atakuwa tayari kukichangia fedha chama hicho wakati mwingine wowote. Ikiwa imebakia wiki moja kabla ya kumalizika kwa muda wa kampeni, Sabodo alitimiza ahadi hiyo ya kuendelea kuisaidia Chadema akisema kuwa lengo lake ni kutoa changamoto kwa chama tawala ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1961 wakati nchi ilipopata uhuru. “Upinzani sio uadui na serikali haiwezi kufanya vizuri bila kuwepo kwa vyama vya upinzani kwa sababu vinatoa changamoto mbalimbali bila ya upinzani ufisadi utaendelea,” alisema Sabodo. Mmiliki huyo wa ukumbi wa kisasa wa sinema unaojulikana kama New World Cinema, aliweka bayana mtazamo wake hasi dhidi ya CCM “Mimi ni kada wa CCM, lakini naona kama siku hizi CCM inapoteza mwelekeo; sio kama naiunga mkono Chadema wala nataka kuhamia Chadema. Mimi ni kada wa CCM, napenda jinsi chama hiki kinavyotoa changamoto kwa serikali. Hii ni sawa, serikali inakuwa kama inakumbushwa, wapinzani ni watu muhimu,” alisema muumini huyo wa falsafa za kiongozi wa kwanza wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata hivyo, Sabodo alisema kuwa nafasi ya Chadema pamoja na vyama vingine vya upinzani kuibuka na ushindi wa kiti cha urais ni ndogo, lakini alisisitiza kuwa uwepo wa vyama hivyo ni changamoto tosha kwa serikali. “Napenda sana mnavyotoa changamoto zenu," alisema Sabodo. "Nafasi yenu ya kushinda urais ni ndogo, nyinyi pamoja na vyama vingine vya upinzani lakini uwepo wenu unaleta ushindani na kuiweka serikali sawasawa," alisema Sabodo, Aliongeza kusema: “Mimi huwa natoa fedha kwa chama hiki, na hii si mara ya kwanza na hiyo haimaanishi kama niko upinzani, bali naangalia chama kinachofanya vizuri kisiasa.” Mchango huo ambao ulikabidhiwa kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ni sehemu ya jitihada mpya kutoka kwa wadau wa siasa kuviwezesha vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikisumbuliwa na ukata kutokana na kutokuwa na vyanzo vya uhakika wa fedha. Vyama vingi vinategemea fedha zinazotolewa kwa hisani na viongozi au wanachama wake kutokana na ruzuku vinavyopata kutoka serikali kuwa ndogo. Ruzuku hutokana na kiasi cha wabunge wanaoingia bungeni na kutopata kura za kutosha kwenye kinyang'anyiro cha urais. Lakini CCM imekuwa ikifaidi ruzuku kutokana na kufanya vizuri kwenye uchaguzi huku wafanyabiashara wakitoa misaada mikubwa ya hali na mali kwa chama hicho tawala. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mbowe alipongeza kitendo cha Sabodo kutoa msaada huo wa fedha kwa Chadema na kuwataka wafanyabiashara maarufu kutosita kuvichangia vyama vya upinzani. "Wengi wanahisi kuwa wakichangia upinzani wataonekana kama wanakisaliti chama tawala, wanachotakiwa kuiga ni hiki anachokifanya Sabodo," alisema Mbowe. Mbowe, ambaye pia ni mfanyabiashara na kwa sasa anagombea ubunge wa Jimbo la Hai, alisema fedha hizo zitakisaidia chama hicho kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. "Hizi fedha zitatusaidia sana hasa kwa wagombea wetu wa nafasi mbalimbali... kwa kweli tunashukuru sana kwa mchango huu; tunashukuru sana," alisema Mbowe ambaye mwaka 2005 aligombea urais. Mbowe alisema Sabodo ni kielelezo cha mfanyabiashara safi na mfano wa kuigwa kwa wafanyabiashara wengine kwani amekuwa mstari wa mbele kusaidia watu bila kujali itikadi zao. Mbali na kutoa fedha hizo, Sabodo pia alitoa dola 20,000 za Kimarekeni kwa ajili ya kuwasaidia watoto wadogo 10 wanapelekwa na Lions Club nchini India kutibiwa maradhi ya moyo. Chadema imeichangia klabu hiyo Sh10 milioni. “Watu wajitokeze kuchangia hasa watu wenye matatizo kama hawa watoto,” alisema Sabodo. Mwenyekiti wa Lions Club, Frank Goyayi alisema kuwa watoto hao waliotarajiwa kuondoka jana alasiri watapatiwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya Fortis Escortis iliyopo New Delhi. |