Monday, June 06, 2016

MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI, (WCF), WAPONGEZWA NA SSRA KWA KUWAFIKIA WADAU MUHIMU




MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI, (WCF), WAPONGEZWA NA SSRA KWA KUWAFIKIA WADAU MUHIMU
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka akitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya siku tano kwa madaktari wanaotoka mikoa ya kanda ya ziwa kuhusu ajali na magonjwa yanayotokana na kazi Jijini Mwanza. Bi. Isaka alisisitiza umuhimu wa WCF na madaktari kufanya kazi pamoja ili waweze kulipa fidia stahiki kwa wafanyakazi wote kutoka sekta Binafsi na Umma. Wengine pichani kutoka kushoto ni Afisa Utumishi Mkuu, Mkoa wa Mwanza, Bw. Salvatory KyaKyarwenda, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo, Bw. Emmanuel Humba.

NA K-VIS MEDIA, MWANZA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Bi Irene Isaka ameipongeza Bodi ya Wadhamini na Mkuurgenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), kwa kuweza kuwafikia wadau wake muhimu kwanza kabla ya kuanza kutoa Fidia kwa Wafanyakazi. 

Bi Isaka aliyasema hayo leo Juni 6, 2016 wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa madaktari 124 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenye ukumbi wa jengo la PPF Plaza jijini Mwanza.Aidha, amesema kuwa sasa hivi wafanyakazi wasifanye kazi kwa wasiwasi kwani kuna chombo maalumu ambacho ndiyo kinga na msaada wao endapo watapatwa na majanga katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Pia Bi. Isaka ametoa wito kwa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), na madaktari kote nchini kufanya kazi pamoja ili waweze kulipa fidia stahiki kwa wafanyakazi wote kutoka sekta Binafsi na Umma.

Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, ni taasisi ya Serikali iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu, na ulianzishwa kwa sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi namba 20 ya mwaka 2008. Lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha Mfanyakazi anapata fidia stahiki kutokana na kuumia kazini au magonjwa yatokanayo na kazi na kwa wanafamilia kupokea fidia kwa niaba ya mwenza wao aliyefariki akiwa kazini.

Mafao yatolewayo na Mfuko huo ambayo kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Masha Mshomba ni pamoja na Fao la matibabu, fidia ya ulemavu wa muda, fidia ya ulemavu wa kudumu, Fidia ya huduma ya marekebisho (Rehabilitation services), Fedha za uangalizi wa mara zote, (Constant attendance care grant), Fedha za mazishi, na fidia kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki akiwa kazini au kutokana na maradhi yaliyosababishwa na kazi aliyokuwa akifanya. "Mfuko utaanza kutoa mafao ya kwanza kabisa tangu uanzishwe kuanzia mwaka wa fedha unaoanza Julai, 2016/2017." Alisema Mkurugenzi Mkuu, Bw. Masha Mshomba.Mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa WCF na Shirika la Kazi Duniani, ILO. 
Mwenyeketi wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Emmanuel Humba akitoa hotuba yake.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, akizungumza mwanzoni mwa mafunzo hayo.
Baadhi ya Madaktari, wakufunzi kutoka ILO wakifuatilia maelezo ya utangulizi
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo
Mkurugenzi Mkuu, Bw. Masha Mshomba, akifafanua baadhi ya mambo kwa waandishi wa habari
Picha ya pamoja
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii, (SSRA), Irene Isaka (kulia), akisalimiana na mtaalamu wa ajali na magonjwa yanayosababishwa na kazi kutoka Shirika la Kazi Duniani, (ILO), Dkt. Jacque Palletier