Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali
Mohamed Shein(pichani), ameiagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha,
Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani
ya wiki moja kwa ajili ya kununua meli kubwa mpya ya abiria wapatao 1000
na yenye uwezo wa kuchukua mizigo ya tani 100.
Dk.
Shein ametoa agizo hilo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na uongozi
wa Shirika la Meli pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambapo pia
kikao hicho kilihudhuriwa na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na
Mawasiliano na Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango
ya Maendeleo.
Katika
kikao hicho maalum Dk. Shein ameiagiza Wizara hiyo kutafuta fedha hizo
kutokana na vianzio vya ndani au nje ya nchi ama kutokana na taasisi
zinazohusiana na mambo ya fedha.
Alieleza
kuwa katika kipindi kisichozidi miezi miwili ujumbe maalum uende kwa
Kampuni zinazotengeneza meli nchini Korea Kusini, China au Japan kwa
ajili ya kuwasilisha fedha za utangulizi kwa ajili ya ujenzi wa meli
hiyo.
Mapema
uongozi wa Shirika la Meli, ulimueleza Dk. Shein kuwa kwa kawaida
ujenzi wa meli yenye ukubwa huo, huchukua mwaka mmoja kukamilika.
Kikao
hicho ambacho kilikuwa na lengo la kuangalia mwelekeo na Mipango ya
Shirika la Meli pia, kilijadili hali halisi ya meli za Shirika la Meli
na baadae kujadili masuala ya ununuzi wa meli mpya itokayowaondoshea
usumbufu wa usafiri wa baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja,
Pemba na Tanzania Bara.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.