Hukumu ya leo imeibua mambo mazito ambapo Lema amesema kuwa anajua
amevuliwa ubunge kwa shinikizo kutoka Ikulu hasa baada ya kuwa amekataa
ombi la mmoja wa viongozi wakuu wa serikali wakati huo la kutaka agombee
nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi kwa ahadi ya kumpa cheo
kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada kutolewa kwa hukumu hiyo,
Lema mwaka 2007 aliitwa na kiongozi huyo ili akubali ombi hilo na alimpa
watu watakaomsaidia kwenye kampeni zake lakini hakukubaliana
naye.Alisema kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 aliitwa tena na
kuombwa amuunge mkono mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, ambapo
wangemtafutia Lema nafasi ndani serikali, lakini alikataa tena hatua
ambayo anaamini ilisababisha chuki.
Aliongeza kuwa sababu nyingine iliyoongeza chuki dhidi yake na serikali,
ni hatua yake ya kukataa kushiriki katika mapokezi ya viongozi wa
kitaifa waliotembelea Arusha akiwemo Rais Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, na kubwa zaidi kutomtambua meya wa jiji la Arusha Gaudence
Lyimo.Katika kuthibitisha madai yake hayo, Lema alisema kuwa alianza
kupata taarifa za kushindwa kwake katika kesi hiyo kutoka kwa watu
mbalimbali kabla ya hukumu ya jana.
Aliwataja waliowahi kumjulisha kushindwa kwake kuwa ni pamoja na baadhi
ya wabunge wa CCM, maafisa usalama wa taifa na marafiki zake muhimu
walioko serikalini.Aliwataja waliomtaarifu kuanguka kwake kuwa ni pamoja
na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nnauye, Mweka Hazina wa chama hicho tawala Mwigulu Mchemba na
ofisa usalama mmoja wa ngazi ya juu (jina linahifadhiwa).Alisema kuwa
hata walipokuwa kwenye harakati za kampeni jimbo la Arumeru Mashariki
Mwigulu Nchemba alisikika akimwambia kijana mmoja aliyeshiriki kura za
maoni ndani ya CCM kugombea ubunge jimbo la Arusha Mjini kuwa ajiandae
kwa uchaguzi wa Arusha Mjini kwani mahakama itatengua ubunge wake
(Lema).“Nilipokuwa najiandaa asubuhi kwenda mahakamani nilipigiwa simu
na mbunge wa Kawe Halima (Mdee) ambaye aliniambia amepata taarifa kuwa
navuliwa ubunge na katibu wetu mkuu (Dk. Willbrod Slaa) alinipigia
kunieleza hivyo hivyo na walinitaka nijipe moyo,”
alisema Lema.
Lema alisema hata alipopita kwenye ofisi yake ya ubunge iliyoko jengo la
mkuu wa wilaya alikuta magari ya polisi karibu 10 yaliyokuwa na polisi
wengi wenye silaha.Alisema ulinzi mkali na kuzuiwa kwa watu mahakamani
kwa kuweka mkanda wa njano kuzunguka majengo ya mahakama, kulithibitisha
kuwa tayari watendaji wa serikali na vyombo vya dola walijua
kitakachoamriwa.“Kitu walichofanya leo ni cha kusikitisha, maana
haiwezekani kesi iliyosikilizwa kwa miezi karibu mitatu jaji akatoa
hukumu kwa muda mfupi kiasi kile.
Wao wana dola sisi tuna Mungu,” alisema.Mbunge huyo aliwaambia mamia ya
watu waliomsindikiza kwa maandamano kutoka mahakamani hadi zilipo ofisi
za CHADEMA mkoa kuwa hukumu hiyo imeendeleza ari yake ya kupigania haki
kwa vile ubunge kwake ulikuwa ni utumishi na si vinginevyo hivyo kwa
sasa ataendeleza harakati za kudai haki mpaka kieleweke.“Safari ya
ukombozi ilianza zamani wengine walikufa wengine walipoteza viungo vyao
lakini safari inaendelea, msiogope ninyi mlio wengi, maana mkiogopa mimi
nitaogopa zaidi lakini nawatia moyo msiogope kuweni jasiri haki haiwezi
kudhalilishwa,” alisema Lema.“Tafsiri niliyoipata mahakamani ni kuwa
wametengua matokeo yangu ya ubunge; mtu leo asiumizwe yeyote unayekutana
naye leo ni kura yetu, kila mtu ameumia kwa sababu mlipiga kura
mkachunga na tukashinda, wao wana jaji wa mahakamani sisi tuna jaji wa
mbinguni.”
Source: Jamii Forum