Friday, April 01, 2016

Benki ya Exim yawapongeza washindi wa mbio za magari


Benki ya Exim yawapongeza washindi wa mbio za magari
Mshindi wa kwanza wa mbio za magari za Vaisakhi Rally 2016 Bw Gurjit Singh (kulia) na msoma  ramani wake Bw Shameer Yusuf wakiwa wameshika vikombe vyao vya ushindi baada ya kumalizika kwa mbio hizo zilizofanyika mkoani Moshi hivi karibuni. Kufuatia ushindi huo washindi hao walitoa pongezi kwa wadhamini wao Benki ya Exim Tanzania kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo.

 Benki ya Exim Tanzania imepongeza timu ya mbio za magari ya Hari Singh kufuatia ushindi iliyoupata hivi karibuni kwenye mbio za magari za Vaisakhi zilizofanyika mjini Moshi ambapo timu hiyo imeweka rekodi ya kushinda mbio hizo kwa miaka tatu mfululizo.

Timu hiyo inayodhaminiwa na Benki ya Exim Tanzania inaundwa na dereva wa kitanzania Gurjit Singh Dhani pamoja na msaidizi wake Shameer Yusuf. Timu hiyo ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mbio hizo baada ya kutumia muda wa 01:23:36 huku ikitumia gari aina ya Subaru GVB2015.

Akitoa pongezi kwa niaba ya benki mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mwakilishi wa benki hiyo Bw Lameck Charles alisema mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na uwezo mkubwa ulioonyeshwa na timu hiyo sambamba na uwezo mkubwa wa gari iliyotumiwa na timu hiyo.

"Exim kama wadhamini wa timu hii tunachukulia ushindi huu kama mafanikio yetu pia na ni zawadi ya msimu wa Pasaka. Uwezo mkubwa wa timu hii ukichagizwa na udhamini mzuri kutoka Benki ya Exim ndio chachu ya mafanikio haya na ndio maana tunaahidi kuendelea kushirikiana na timu hii tukilenga mafanikio zaidi,'' aliongeza mwakilishi mwingine Bw Philip Mtei.

Akizungumzia ushindi huo dereva Gurjit alisema pamoja na uwezo mkubwa wa timu yake pia ulichagizwa na maandalizi mazuri, ubora wa gari pamoja na ushirikiano mzuri alioupata kutoka kwa wadhamini hao.

"Ushindani ulikuwa ni mkubwa na changamoto pia zilikuwepo ila mwisho wa siku tunashukuru sana kwa ushindi wetu ambao tunauelekeza kwa wadau wetu wakiwemo ndugu, mashabiki na wadhamini wetu hususani benki ya Exim,'' alisema mshindi huyo.