Na Mwandishi Maalum . New York
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio jipya ambalo pamoja na mambo mengine limeiongezea kwa mwaka mmoja Misheni ya kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO ).
Sambamba na kuiongezea mwaka MONUSCO, Baraza la Usalama pia limesitisha zoezi la kupunguza walinzi wa Amani 1,700 kama ilivyopendekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Huku Azimio hilo likitamka bayana kuwa MONUSCO inatakiwa kuwa na walinzi wa Amani wasiopungua 19,815, waangalizi 760, pamoja na polisi 1,050.
Ndani ya MONUSCO kuna Brigedi maalum ijulikanayo kama Force Intervention Brigade (FIB) yenye mamlaka nguvu ya kuyashughulikia makundi ya waasi yenye silaha. Brigedi hii inaundwa na walinzi wa amani kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.
Kwa mujibu wa Azimio hilo jipya lililopitishwa na wajumbe 15 wa Baraza la Usalama, uamuzi wa kuiongezea muda wa mwaka mmoja MONUSCO hadi Machi 31,2017, pamoja na kutotoa baraka za kupunguzwa kwa walinzi wa Amani kunatokana na taarifa za kuzorota kwa hali ya usalama hususani katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Rais mwezi Novemba mwaka huu na tayari kuna taarifa za kuwapo kwa sintofahamu miongoni mwa makabila kutokana na tofauti za kisiasa, kuongezeka kwa makundi ya waasi wenye silaha, kuzorota kwa hali ya kibinadamu hali inayoitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa kwamba kunauwezekano wa kutokea machafuko.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupitia Azimio hilo, limeionya Serikali ya DRC kuhusu kuchelewa kwa maandalizi ya uchaguzi wa rais, huku likitoa wito kwa serikali wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, na makosa ya uhalifu wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu.
Vile vile Baraza la Usalama limetoa wito kwa serikali na wadau wengine pamoja na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi ( CENI) wa kuhakikisha uwazi kuhusu mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa kalenda ya uhakika ya uchaguzi.
Aidha serikali imetakiwa kutenga bajeti ya kutosha kwaajili ya uchaguzi na kuweka maadili ya uchaguzi na kuchukua hatua za kuboresha daftari la wapiga kura pasipo kuchelewa.
Kuhusu makundi ya waasi wenye silaha, wajumbe wa Baraza la Usalama wametoa wito wa kutaka kurejeshwa mapema iwezekanavyo operesheni ya pamoja kati ya MONUSCO na Jeshi la DRC ( FARDC) dhidi ya makundi hayo ya waasi hususani kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda ( FDLR).Makundi mengine ya waasi na ambayo yameendeleza matukio ya mauaji ya raia wasio na hatia na ambayo pia yanatakiwa kushughulikiwa ni pamoja na kundi la ADF, Mai Mai na LRA
Azimio hilo lenye kurasa 15 pia limetilia mkazo kuhusu ulinzi wa raia, ulinzi wa watoto na linakemea vikali kuhusu vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.