Monday, March 30, 2015

Rais Mugabe ' Amlilia ' Nyerere......Aimwagia Sifa Tanzania


Rais Mugabe ' Amlilia ' Nyerere......Aimwagia Sifa Tanzania

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amefungua mkutano wa tatu wa pamoja baina ya viongozi vijana wa Afrika na China, akitumia muda mwingi wa hotuba yake 'kumlilia' Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
 
Mbali ya Nyerere, Rais Mugabe pia alitumia mkutano huo kuwakumbuka waasisi wa mataifa mbalimbali ya Afrika, huku akiimwagia sifa Tanzania kwa mchango mkubwa iliyotoa kwa ukombozi wa Bara la Afrika.
 
Akiwahutubia vijana hao kutoka mataifa ya Afrika na China, Rais Mugabe ameonya juu ya kasi ya kurejea kwa ukoloni kwa mlango wa nyuma na amewaagiza vijana kusimama imara, vinginevyo Afrika itaangamia.
 
Mwenyekiti huyo wa AU, aliyasema hayo katika ukumbi wa Hoteli ya Ngurdoto iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha, alipozindua mkutano huo wa tatu, unaoendeleza mikutano miwili ya awali, wa mwaka 2011 uliofanyika Afrika na wa pili uliofanyika Beijing, China 2012.
 
Kiongozi huyo anayebakia kuwa mwasisi aliyesalia katika ukombozi wa bara la Afrika alisema kamwe katika historia yake hatamsahau Mwalimu Nyerere na aliwaomba vijana kuzingatia falsafa na matendo yake.
 
Alisema pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Nyerere na waasisi wengine katika ukombozi wa bara la Afrika, lakini hivi sasa hali si shwari kwani kuna kasi kubwa ya kurejea kwa ukoloni kupitia mlango wa nyuma kwa kile alichokiita ukoloni mamboleo na utandawazi.
 
"Kisiasa tunaweza kusema tumekamilisha Uhuru wa Bala la Afrika lakini si kweli, bado tunayo kazi ya kufanya na kazi hiyo ni lazima muifanye nyie vijana," alisema na kusisitiza Afrika inaweza kujitawala na kujiletea maendeleo yake bila kutegemea misaada kutoka mataifa ya Magharibi.