Friday, January 30, 2015

Pinda aahidi kumshughulikia Katibu Tarafa Kariakoo kwa kunyang’anya mali za wafanyabiashara kwa kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana


Pinda aahidi kumshughulikia Katibu Tarafa Kariakoo kwa kunyang'anya mali za wafanyabiashara kwa kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana Waziri Mkuu, Mizengo            Pinda 

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza watendaji katika Manispaa na Jiji waliohusika kunyang'anya mali za wafanyabiashara mbalimbali kwa kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana badala ya kupeleka kunakoruhusiwa kuchukuliwa hatua huku akiahidi kumshughulikia Katibu Tarafa wa Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na wafanyabiashara na kuangalia njia nzuri ya kufanya biashara ili kuondoa vurugu baina yao na vijana.

Pinda aliyasema hayo jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu alipojibu swali la Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu (CCM) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu wanamgambo wanaotumia nafasi ya kusafisha jiji kuwanyanyasa wafanyabiashara na kugawana mali zao huku tatizo kubwa likiwa kwa Katibu Tarafa wa Kariakoo.

Amesema yeye binafsi alitumiwa picha ya watendaji hao wakigawana mali walizowanyang'anya wafanyabiashara wakiwamo mama lishe, jambo ambalo ni kuwanyanyasa na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Waziri Mkuu alikemea kitendo cha watendaji wa jiji na mikoa kutumia kusafisha jiji kunyanyasa wananchi.

Hivyo aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kukaa na wafanyabiashara ndogo na kupanga jinsi ya kuendesha biashara kistaarabu ikiwa ni pamoja na kupanga masoko ya jioni na Jumapili ili wafanye biashara muda mfupi na kuondoka.