Monday, September 24, 2012

Mashindano Ya 32 Ya Shirikisho La Michezo Ya Wizara Na Idara Za Serikali ( SHIMIWI) Morogoro by Mjengwa



Hapa ni patashika kati ya timu ya Netiboli Wizara ya Kilimo (jezi za mchezaji aliyeshika mpira0  VS timu ya Maji leo ambapo  Kilimo ilishinda bao 32- 22.

Wachezaji wa michezo ya aina mbalimbali ya timu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakipita mbele ya jukwaa la mgeni rasmi



Kikosi cha timu ya mpira wa Netiboli Ofisi ya RAS Kilimanjaro , wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukosa mshindani
   Timu ya mpira wa Netiboli ya Ikulu, ikikaguliwa na Mwamuzi , baada ya kumaliza kuikagua timu ya Tume ya Utumishi.

Picha  na habari John Nditi, 

 WAZIRI wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo, Dk Finella Mukangara, amezitaka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zihakikishe zina kuwa na bajeti ya kutosha ya michezo ili kutafsiri dhana zima ya Serilali ya kupenda na kuhimiza michezo kazini. 

Pia amesema ni wajibu wa kila Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ,Vyama vya Michezo na sehemu za jamii kuwajibika kimatendo katika kukuza na kuendeleza michezo. Dk Mukangara alisema hayo Septemba 22, mwaka huu katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mashindano ya 32 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali ( SHIMIWI) kwa mwaka 2012 yanayofanyika Mkoani Morogoro na kuwashirikisha zaidi ya wanamichezo 3,000 kutoka katika timu 63 za Wizara pamoja na Idara za Serikali. 

Hivyo alisema , ni wajibu wa viongozi wote sehemu za kazi kuendelea kusimamia shughuli za michezo na kuhakikisha watumishi wanashiriki kikamilifu michezo ili waweze kujenga na kuwa wakakamavu wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku. “Mashindano ya Shimiwi yana umuhimu wa kipekee kwetu sote , hili ni darasa tosha la vitendo katika nidhamu, mshikamano, burdani , uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja , makundi mbalimbali na Wizara kwaujumla” alisema Dk Mukangara. Waziri Mukangara pia aliupongeza Uongozi wa Shimiwi kwa kuamuzi wake wakuhusisha makundi maalumu yakiwemoi ya watu wenye ulamavu katika michezo hiyo.

 “ Utaratibu huu unaonesha ni kwa kiasi gani mnatambua umuhimu wa kuendeleza michezo kwa watu wenye vipaji bila kuwasahau wenzetu wenye ulemavu na mahitaji maalum …nawapongeza kwa hatua hii” alisema Waziri huyo. Hata hivyo alisema ni matarajio yake kuwa ushiriki wa watu wenye ulemavu utaongezeka mwaka hadi mwaka na kuhusisha aina nyingi za michezo kwa lengo la kuhakikisha vipaji vya michezo vinaibuliwa na kuendelezwa kwa dhati kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine wa Serikali bila kubaguliwa. 

Waziri huyo, pia aliwatahadharisha Wanamichezo hao wa Shimiwi kuwa Ukimwi bado ni tatizo kubwa hapa nchini na kasi ya maabukuzi bado ni kubwa , hivyo ni wajibu wao wasijiruhusu kujenga mazingira hatarishi ya kuambukizana Virusi vya Ukimwi wakati wote wa michezo hiyo.