Na Maimuna Kubegeya SIKU
zote mwanamke awapo mjamzito huwa na matarajio makubwa ya kukipata
kiumbe chake ambacho huwa ni faraja ya pekee maishani mwake.
Lakini
inapotokea mwanamke huyo akashindwa kukipakata kiumbe alichokisubiri
kwa hamu kwa muda mrefu wa miezi tisa, huwa ni msiba … majuto na upweke
wa aina yake.
Hiyo ndiyo hali iwakumbayo wanawake wengi wanaopoteza watoto wao wakati wakujifungua . Zipo sababu chekwa zisababishazo vifo vya watoto wachanga na moja ya sababu hizo ni maumbile ya wanawake wenyewe.
Wengine si tu hupoteza vichanga bali hata maisha yao wenyewe huenda yakawekwa rehani katika kipindi hiki.
Kwa
mujibu wa Hadija Kimwaga, Ofisa Muuguzi na Mkunga kutoka Hospitali ya
Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wanawake wafupi wako katika hatari ya
kupata matatizo wakati wa kujifungua ingawaje si kila mwanamke wa aina
hiyo kwani wapo wengine ambao hujifungua kwa njia ya kawaida.
“Baadhi
ya wanawake walio na urefu ulio chini ya sentimita 150 huwa na nyonga
ndogo. Hivyo, inashauriwa mara watakapokuwa na ujauzito kwenda kwanye
vituo vikubwa vya afya ama hospitali kubwa kwani huko wanaweza kupata
huduma sahihi”, anaeleza.
Anaongeza kuwa na hii ni miongoni mwa
sababu zinazowafanya wataalamu wa afya kuwashauri kufika kwenye vituo
vya afya kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mtoto na afya zao kwa
ujumla katika kipindi hicho.
Kwa wale wanaopata tatizo mara nyingi
njia pekee ya kuwanusuru imekuwa ni upasuaji. Hivyo, ikithibitika kuwa
nyonga za mwanamke husika hajitanuki kwa kiwango kinachohitajika basi
huduma hiyo hutolewa kwa lengo la kunusuru maisha ya mama na
mtoto.Lakini hatari kubwa hutokea pale wanapocheleweshwa anasisitiza.
Pamoja
na kuwa suala la kimo mara nyingi hutegemea na hali ya kijenetiki,
wakati mwingine ufupi husababishwa na ukosefu wa lishe bora wakati wa
utotoni.
Mmoja wa wanawake waliofikwa na msiba wa kupoteza kichanga ni Margreth Mwenda.
Magreth
anasema: “NI siku ambayo siwezi kuisahau maishani kwangu. Ninakumbuka
kuwa ilikuwa mwezi wa Januari mwaka 2000, nikiwa kwenye moja ya kitanda
katika wodi ya wazazi, kwenye Hospitali ya St. Francis Wilaya ya
Kilombero Mkoa wa Morogoro”, anasemaMwenda.
Kwa wakati huo, kitu pekee alichokuwa akitarajia ni kumkumbatia mwanawe ambaye alikuwa akitarajia kujifungua muda mfupi ujao.
“Huwezi
kuamini, mtoto ambaye nilikuwa namsubiri kwa hamu, tena nikimsikia
anavyonipiga mateke tumboni, alifariki muda mfupi kabla ya kujifungua.
Alifia njiani,” anasema mwanamke huyu mwanye umri wa makamo.
“Kwani
nilishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana na nyonga zangu
kushindwa kutanuka. Jambo hilo lilisababisha mtoto kushindwa kushuka
kwenye njia yake ya kawaida’’, anafafanua Mwenda.
“Pamoja na
uchungu nilionao, lakini naweza kueleza kuwa sababu moja wapo
iliyochangia kumpoteza mwanangu, ni kuchelewa kufika hospitalini na
hivyo kupoteza damu nyingi sana kabla ya kujifungua”, anasema kwa huzuni
mama huyo.
Dk. Hassan Saad kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi (Tacaids)anasema kimo kifupi mara nyingi husababisha matatizo
wakati wa kujifungua kutokana tatizo la kushindwa kutanuka kwa nyonga Anasema
tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa mara nyingi lishe duni wakati wa
utotoni hupelekea kudumaa. Jambo linalochangia hupelekea mtoto husika
kuwa mfupi.
Baadhi ya mambo yanayochangia hali hiyo ni ukosefu wa
vitamini D na ukosefu wa mwanga wa jua wa kutosha unaosababisha kupata
matege na magonjwa mengine ya mifupa ikiwamo hilo la kutokuongezeka kwa
nyonga.
“Lishe bora ina nafasi kubwa ya kuongeza kimo na pia kuongeza kimo cha mji wa uzazi” alisema. Imebainishwa kuwa wanawake walio katika tatizo hili kwa sasa, huwa wameathiriwa wakiwa wadogo.
Dk
Maggie Blott, mshauri wa masuala yanayohusu magonjwa ya wanawake,
kutoka Uingereza ameandika kwenye mtandao wake kuwa baadhi ya wanawake
walio na kimo kifupi wana nyonga ndogo, ambazo hushindwa kushindwa
kutanuka wakati wa kujifungua na hivyo kusababisha madaktari kuchukua
uamuzi wa kuwafanyia upasuaji .
“Mara nyingi ili kuokoa maisha ya mama na mtoto, tumekuwa tukitumia njia ya upasuaji”, anaandika daktari huyo. “
Katika nchi zinazoendelea umasikini na ukosefu wa lishe bora kwa
watoto unasababisha watoto hao kukua , wakati mifupa ya wasichana
inakuwa haijakomaa. Hali hii ya kudumaa husababisha matatizo wakati wa
kujifungua na pia fistula”, anasisitiza.
Tatizo hili limekuwa ni la kawaida kwa nchi masikini na hasa kwa wanawake na wasichana walio na hali ya chini kimaisha.
Vifo
vya wajawazito mara nyingi vinasababishwa na matatizo wakati wa
kujifungua na vimekuwa vikiongezeka zaidi katika nchi zinazoendelea
hasa kutokana na huduma duni za afya zinazotolewa hususani na wakunga
jadi. Wakati mwingine mzazi hupoteza damu nyingi sana kabla ya
kujifungua, kutokana na mtoto kukandamiza njia ya uzazi na kusababisha
majeraha yanayosababisha kuvuja kwa damu. Jambo linalosababisha mwanamke
husika kufanyiwa upasuaji.
Ulaji wa chakula bora tangu kipindi cha mimba na baada ya kuzaliwa, ni njia mojawapo ya kuepuka tatizo hili. Kwani ikiwa mama atakula chakula bora wakati wa ujauzito, ni wazi kuwa atajifungua mtoto mwenye afya bora. Mtoto
huyo pia akipata chakula bora wakati wa makuzi yake, ni wazi kuwa
atakuwa katika hali bora kiafya. Hali hiyo huchangia kuondoa udumavu,
unaopelekea hatari wakati wa kujifungua.
Lakini, kwa wanawake
kama Magreth Mwenda hawana jinsi ya kurekebisha maumbile yao, isipokuwa
ni kuhakikisha wanajifungua sehemu salama yenye madaktari wenye ujuzi
wa kutosha.
Pia, kuwapa chakula bora watoto wao pindi watakapojifungua ili kuwaepusha na tatizo kama hilo.
Source: Mwananchi. |