Na Mwandishi Wetu
BADO taifa linaombeleza kifo
cha msanii nyota wa filamu za Bongo, Steven Charles Kanumba kilichotokea
Aprili 7 mwaka huu nyumbani kwake, Sinza, Dar es Salaam.
Kifo cha
msanii huyo kinamhusisha msanii nyota wa kike wa tasnia hiyo nchini,
Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anasemekana aligombana naye kwa mambo ya
mapenzi na kumsukuma.
Lulu alishikiliwa na polisi wa kituo cha
Oysterbay cha jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi kufuatia kifo cha
mpenzi wake huyo.
Hapo ndipo kwenye habari! Kwamba, kumbe marehemu
Kanumba na Lulu walikuwa wapenzi! Ni vigumu kwa watu kuamini au
kukubali, lakini ukweli unabaki kuwa huo.
Baada ya taarifa hizo, timu
ya Risasi Mchanganyiko iliingia kazini ili kuchunguza siri hiyo nzito
iliyodumu kwa takribani zaidi ya miezi sita.
MWANZO WA MAPENZI
Kwa
mujibu wa watu wa karibu na marehemu Kanumba ambao walifunguka baada ya
kifo huku wakiomba kusitiriwa kwa majina yao, wawili hao walianza
uhusiano wakiwa katika safari moja ya sanaa mjini Moshi, Kilimanjaro.
Safari hiyo ilihusisha kundi zima la Bongo Movie Club.
Kanumba ndiye
aliyemtongoza Lulu na kukubaliwa na kuanzia hapo uhusiano wao ulianza
rasmi. Lulu alianza kwenda nyumbani kwa Kanumba bila kipingamizi.
Majirani
wa Kanumba wanakiri kuwa, mara kadhaa Lulu alikuwa akifika nyumbani
hapo na ilifika wakati walikuwa wakipika na kupakua kama mke na mume.
MPANGO WA KANUMBA
Kwa
mujibu wa habari hizo, marehemu kumtaka Lulu kimapenzi hakukuwa kwa
ajili ya kujifurahisha nafsi bali kumuoa kwa ndoa na kuwa mke na mume.
“Lakini
nataka kusema jambo zuri, usidhanie Kanumba alimtaka Lulu ili kumtumia
tu, hapana! Alipanga naye maisha, alishamtamkia kumuoa,” alisema mmoja
wa watoa taarifa.
UTAMBULISHO ULISHAANZA
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti
hili ulibaini pia kuwa, Kanumba alishaanza hatua ya awali ya maandalizi
ya uchumba wao kwa kumpeleka Lulu kwa watu wake wa karibu na
kumtambulisha.
Mtu ambaye kuna uhakika alishakutanishwa na Lulu ni msanii na mama mlezi wa wasanii Bongo, Husna Poshi ‘Dotnata’.
Inadaiwa
kuwa, Kanumba alifunga safari na Lulu hadi nyumbani kwa Dotnata, Ubungo
ya Riverside, Dar ambapo aliweka wazi uhusiano wake na msanii huyo na
mipango ya kumuoa.
Habari za ndani zinadai kuwa Dotnata, mbali na kushtuka
alimuuliza Lulu kama atatulia baada ya kuwa na Kanumba kwa lengo la
kufunga ndoa ambapo msanii huyo alisema ameshatulia.
Aidha, habari zinasema kuwa, Kanumba alimhakikishia Dotnata kuhusu uhusiano wake na Lulu huku akisisitiza si wa kuchezeana.
Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya kuongea na Dotnata kuhusu madai hayo ambapo alikiri.
“Ni
kweli, Kanumba aliwahi kumleta Lulu kwangu, akaniambia ameamua kuwa
naye na mipango yao haikuwa mibaya kwani ilikuwa kuja kufunga ndoa.
Nilimuuliza Lulu kama atatulia, akanijibu ameshatulia,” alisema Dotnata.
MASHARTI 4 ALIYOMWEKEA LULU ILI KULINDA PENZI LAO
Wakiwa
ndani ya mapenzi motomoto, inadaiwa Kanumba alihisi penzi lao lingeweza
kuvuja kabla ya muda aliotaka yeye, hivyo alimpa masharti manne Lulu
ili kulilinda penzi hilo na mikono ya mapaparazi.
SHARTI NAMBARI MOJA
Lulu
hakutakiwa kuzungumza na mwandishi yeyote wa habari kuhusu uhusiano wao
na kama ni kusema, basi msemaji mkuu angekuwa Kanumba mwenyewe.
“Lulu
aliambiwa kuwa asije akalianika penzi lao kwa watu, hasa waandishi wa
habari. Na kama ni kuliweka wazi, basi mwenyewe ndiye angekuwa msemaji
mkuu,” kilisema chanzo chetu.
SHARTI NAMBARI MBILI
Kanumba
alimwambia Lulu anapokwenda na kutoka nyumbani kwake, alitakiwa kupanda
taksi moja yenye ‘tinted’ inayopaki Kituo cha Vatican City Hotel, Sinza.
Kituo hicho kipo umbali wa mita kama thelathini kutoka nyumbani kwa marehemu.
SHARTI NAMBA TATU
Lulu
alitakiwa kuachana na tabia za zamani, hasa za kupatikana kwenye vilabu
vya usiku huku akiwa amelewa, sambamba na kuepuka vituko mbalimbali
ambavyo vingeweza kumchafua katika jamii.
“Kama vile haitoshi, Lulu alipigwa marufuku kwenda kwenye vilabu vya usiku akiwa peke yake au na kampani mbaya.
“Pia akaambiwa aepuke vituko vya hapa na pale ambavyo vikinaswa
na waandishi wa habari na kuandikwa vitamharibia sifa katika jamii,”
kilisema chanzo.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, kwa kutii sharti
hilo ndiyo maana miezi ya hivi karibuni, Lulu alikauka kwenye vyombo vya
habari.
SHARTI NAMBA NNE
Kanumba, kwa vile alishajua mipango
ya baadaye na Lulu ni kuishi pamoja, alimtaka aachane na wanaume wake wa
zamani na kuanza kurasa mpya na yeye, jambo ambalo Lulu alilitii.
Lakini
katika yote, inaonekana marehemu alisahau kuweka masharti juu ya
matumizi ya simu kwani ndiyo tatizo lililoibukia hapo na kusababisha
kifo.
Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.