Monday, May 23, 2016

MWENYEKITI WA MTAA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MWANZA



MWENYEKITI WA MTAA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MWANZA
MWENYEKITI wa Mtaa wa Bulale wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Alphonce  Nyinzi  (48) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika wakati akielekea nyumbani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 22 mwaka  huu majira ya  saa 2 usiku.

Msangi amesema kuwa marehemu aliekuwa akifahamika  kwa jina maarufu "msukuma" mfanyabiashara na mkazi wa bulale aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na kutokea chini ya kwapa upande wa kulia na watu wawili wasio fahamika pamoja na risasi hiyo kumjeruhi  Neema Marangula (23) Mkazi wa Bulale katika Kiganja cha mkono wa kulia.

 Amesema kuwa wakati Mwenyekiti huyo akitoka  kwenye kikao alichofanya na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mtaa wa Bulale akiongozana na wajumbe wawili alikutana na Neema Marangula akiwa na mume wake ambao walikua wanawafuata marehemu na Balozi kwa ajili ya kuzungumzia mzozo wa ndani ya ndoa yao kwa hiyo walikua wanahitaji kusuluhishwa.

Mwenyekiti  huyo (marehemu) na wajumbe wake wawili wakiwa pamoja na Neema pamoja na mumewe wakiwa wanajadili tatizo hilo hapo barabarani mara ghafla wakatokea watu wawili ambao walikua wakipita barabarani na kuwaambia mko chini ya ulinzi na mmoja wao akatoa bunduki na kumpiga risasi mwenyekiti huyo  ambaye alianguka chini huku wenzake wakikimbia kujiokoa kutoka eneo hilo lakini pia wale wahalifu  wakakimbia na kutokomea gizani vichakani.

Amesema wananchi wa eneo hilo  ambapo mwenyekiti aliuawa walijitokeza kwa msaada wa kumsaidia walimchukua na kumkimbiza hospitali kwa matibabu lakini alifariki dunia wakiwa njiani. majeruhi Neema Marangula amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Mwili wa marehemu  umehifadhiwa katika  Hospitali Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi wa daktari, chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika pamoja na  uchunguzi tukio hilo bado unaendelea.

Msangi  amewaomba  wananchi wenye taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo zitakazo saidia kufanikisha kukamata wahusika wazitoe  polisi lakini pia kutoa ushirikiano kwa viongozi wao na kuhakikisha wanatengeneza makazi salama huko wanapoishi na maeneo ya shughuli zao na  msako mkali unafanyika na kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa.