Saturday, April 23, 2016

RC . MONGELLA ATOA SAA 24 KOMPYUTA YA HALMASHAURI YA UKEREWE ILIYOIBWA IPATIKANE



RC . MONGELLA ATOA SAA 24 KOMPYUTA YA HALMASHAURI YA UKEREWE ILIYOIBWA IPATIKANE
Na Afisa habari RS MWANZA.
Mkuu wa mkoa wa MWANZA John Mongella (pichani) ametoa saa 24 kwa kamanda wa Polisi Wilaya ya Ukerewe Ally Mkaripa, kuhakikisha wanaitafuta hadi kuipata komputa iliyoibwa usiku wa kuamkia April 22, 2016 kwenye chumba kinachotumika na mifumo ya ukusanyaji mapato  na uaandaji wa malipo ya Halmashauri (EPICOR)
Mhe. Mongella ametoa agizo hilo wakati  akizungumza kwenye kikao cha kujitambulisha kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri,ambapo taarifa za awali zilionesha kutokea kwa wizi wa komputa moja iliyofungwa kwenye chumba cha mifumo ya komputa ambayo ndio hutumika kuandaa malipo mbali mbali ya halmashauri.
"OCD kesho nitakwenda kanisani asubuhi, ikifika saa 8.00 mchana nataka taarifa niikute mezani kwangu, vinginevyo hatutaelewana", amesema Mongella na kuongeza sisi tunajua nini chakufanya kama kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa lakini na wewe tumia mbinu zako kuweza kubaini wapi ilipo kompyuta hiyo.
Akizungumza kando ya ukumbi wa mikutano wa halmashauri, kaimu mhazini wa halmashauri hiyo Baraka Munuo, alidai kupokea taarifa za kupotea kwa Komputa hiyo kutoka kwa  afisa TEHAMA wa halmashauri ya Ukerewe akimuelezea upotevu huo.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa wa MWANZA, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya  ukerewe,, kupitia mafaili na kubaini watumishi waliofanya kazi katika kituo hicho kwa muda mrefu, jambo ambalo mkuu wa mkoa amedai linachangia watumishi kufanyakazi kwa mazoea.
"Mkurugenzi nakuagiza pitia mafaili ya watumishi ili kubaini wote waliokaa katika kituo hiki kwa muda mrefu. Haiwezekani mtu amekaa hapa miaka ishirini na moja halafu uniambie kwamba atakuwa na maarifa mapya, hapana" alisema Mongella na kuongeza, Sasa nakuagiza pitia mafaili yao na kama kuna mtumishi aliye kaa kwa zaidi ya miaka kumi atafutiwe kituo kingine.
Awali akisoma taarifa ya wilaya hiyo, mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Joseph Mkirikiti,alimwambia mkuu wa mkoa kuwa hali ya ulinzi na usalama ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za maendeleo huku akisema wilaya imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu kilicho kuwa kimepiga kambi katika Wilaya hiyo kwa zaidi ya miezi 6.
Mkuu wa mkoa wa yupo katika ziara yakujitambulisha na hii ikiwa ni wilaya yake ya saba,Mara baada yakutembelea wilaya za Misungwi, Magu, Nyamagana, Ilemela na Kwimba na hii ya Ukerewe inakuwa wilaya ya saba huku akiwa amebakiza wilaya moja ya Sengerema yenye halmashauri za Buchosa na Sengerema yenyewe.