Sunday, November 29, 2015

Watakaokwamisha juhudi za Rais Dkt. Magufuli katika sekta ya elimu kukiona - Masaju



Watakaokwamisha juhudi za Rais Dkt. Magufuli katika sekta ya elimu kukiona - Masaju
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju akiongea na wazazi, wanafunzi na Viongozi wa Shule za wanawake na wanaume za Feza katika mahafali ya shule hiyo yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam na kusisitiza katika umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju akitoa veti kwa baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika maaeneo ya Uongozi, Usafi na katika Elimu katika kipindi cha miaka minne ya masomo yao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wahitimu wa kidato cha nne wa shule za Fedha.
Picha/Habari na Hassan Silayo
Wananchi wameshauriwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kuendeleza sekta ya elimu kwa maslahi na maendeleo ya watoto na nchi kwa ujumla.


Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju wakati wa Mahafali ya Shule za Sekondari za Wavulana na Wasichana za Feza  Jijini Dar es Salaam.

Bw. Masaju alisema kuwa anatambua Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli imeamua na kuelekeza kwamba kuanzia Januari 2016 elimu itolewe bure kuanzia ngazi ya awali (Kindergarten) hadi kidato cha nne ikiwa ni njia ya kuwafanya watoto wa shule za msingi au watoto waliofalu na kupata nafasi ya kusoma elimu ya sekondari kutokusoma.

Masaju alisema kuwa Asiwepo mtu atakayesababisha mtoto kukosa haki yake ya kupata elimu kwa sababu yoyote ile ikiwemo kuwaozesha watoto, kuwapa ujauzito, kuwaficha majumbani, kuwaachisha masomo, kuwatorosha shule, utoro kwani kama nilivyoeleza awali kufanya hivyo ni kutenda kosa la jinai chini Sheria ya Elimu na Kanuni zake hivyo serikali itachukua hatua dhidi yake.

"Kama tunavyofahamu Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli imeamua na kuelekeza kwamba kuanzia Januari 2016 elimu itolewe bure kuanzia ngazi ya awali (Kindergarten) hadi kidato cha nne, hivyo asiwepo mtu atakayekwamisha juhudi hizi kwa njia yoyote ile kwani ni kuwanyima watoto haki yao ya kikatiba kwani Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo" Alisema Masaju.

Pia Bw. Masaju alizitaka shule na taasisi za elimu kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote kutumia haki ya uhuru wa kuabudu kulingana na imani za dini zao kwa kupanga mitihani au vipindi kwa muda au siku za kuabudu kwani ni kukiuka masharti ya Ibara ya 19 inayotoa haki ya uhuru wa kuabudu.

Aidha Masaju alizipongeza sekta binafsi za elimu kwa kutoa mchango mkubwa katika utoaji wa elimu hapa nchini kwa kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya msingi na elimu ya sekondari; kuongeza vyanzo vya kodi na hivyo kukuza uchumi na huduma za kijamii kutokana na kodi inayolipwa na shule zinazotoa huduma ya elimu; kutunza na kuendeleza utamaduni wa Kitanzania kwa kuwezesha watoto kusoma hapa Tanzania badala ya kupelekwa kusoma nje ya nchi; na kuongeza ajira kwa walimu na watu wa kada mbalimbali wanaoajiriwa na shule binafsi