Thursday, April 02, 2015

Mtikila afuta kesi ya Mahakama ya Kadhi mahakamani


Mtikila afuta kesi ya Mahakama ya Kadhi mahakamani
Mchungaji Christopher Mtikila

Mchungaji Christopher Mtikila (pichani), ameiondoa mahakamani kesi ya kupinga serikali kupeleka bungeni Muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, baada ya jopo la majaji kumshauri kufanya hivyo kutokana na taarifa za kuondolewa bungeni.
 
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Watendaji wakuu wa serikali akiwamo Warizi Mkuu, Mizengo Pinda.
 
Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Mwenyekiti, Richard Mziray, akisaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Said Kihio katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
 
Jaji Kaduri alihoji kama kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo mahakamani wakati Ikulu imesema serikali haina mpango wa kuanzisha Mahakama hiyo na Bunge limeshauondoa muswaada huo.
 
Alisema kusikiliza kesi inayozungumzia muswada huo uliondolewa bungeni haina maana na hata maamuzi yake yatakuwa hayana mashiko kisheria.
"Watanzania hatujaelimishwa nini kinaanzishwa na kitakuwa na majukumu gani hali ambayo imetuacha tumechanganyikiwa … kuna mgawanyiko mkubwa mara maaskofu wanasema hili mara wabunge na wananchi pia wanasema mengine ili mradi tu kila pande inashindwa kuelewa nini haswa kipo mbele yetu," alisema Mwenyekiti na kuongeza:
 
"Tuache kwanza wananchi wapate elimu ya kutosha ili wajue nini kinajadiliwa na hata kitapopitishwa wajue kuna faida gani wanapata." 
 
Akizungumza na Majaji hao, Mtikila alidai kuwa lengo la kufungua kesi hiyo ni pamoja na kunyoosha mkondo wa sheria kwa sababu wapo wanaovunja sheria na kupuuza kazi za Mahakama.
 
Jopo hilo lilimshauri Mtikila kwamba kama ana nia ya kuendelea na maombi mengine yaliyopo kwenye kesi hiyo aiondoe mahakamani  na kwenda kuandaa upya maombi yake yasiyokuwa na kipengele cha Muswada wa Mahakama ya Kadhi.
 
Mtikila alikubaliana na ushauri wa jopo hilo liliondoa kesi iliyosajiliwa kwa namba 14, ya mwaka huu.
 
Akizungumza nje ya Mahakama, Mtikila alisema baada ya kuliondoa shauri hilo mahakamani anatarajia kuandaa maombi mapya dhidi ya Waziri Mkuu, Pinda na wenzake ili waende waieleze mahakama kwa nini waliandaa muswada huo.