Tuesday, February 24, 2015

MWANAMKE HUYU NI SHUJAA



MWANAMKE HUYU NI SHUJAA

WIKI hii mwanamke Ester Bahati (30), alijeruhiwa vibaya na sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando huku akiwa na hali mbaya, baada ya kupambana na watekaji waliokuwa na silaha mbalimbali za jadi, kwa ajili ya kumuokoa mtoto wake mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati.


Mtoto huyo aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi sita ambaye kwa sasa ni marehemu, alitekwa na watu wasiojulikana na baadaye mwili wake kukutwa umefukiwa huku umenyofolewa miguu na mikono.
Licha ya kuwa mtoto huyo kwa sasa ni marehemu, huku mama yake akiwa mahututi, lakini mama huyo alijitahidi kupambana kadri ya uwezo wake kwa lengo la kumuokoa mtoto wake.
Wakati mama huyo akipambana na watekaji hao, jambo la kushangaza baba mzazi wa Yohana, Bahati Misalaba, mkazi wa wilaya ya Chato alikuwa akiangalia huku akiota moto.
Tayari anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi. Lakini katika hali ya kawaida tukiwa tunaelekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, wanawake wote tunapaswa kumuombea mwanamke mwenzetu ambaye kwa sasa yuko hospitalini kutokana na kupigania maisha ya mtoto wake.
Hakika mwanamke huyo ni shujaa kwani katika hali ya kawaida ni dhahiri angeweza kukimbia na kumuacha mtoto wake akichukuliwa kirahisi na wateka nyara, lakini hakuweza kukubali kirahisi na sasa anauguza majeraha ya kumuokoa mwanawe.
Ni dhahiri kuwa mwanamke huyo anapaswa kuigwa na wanawake wote kwa kuhakikisha tunapambana hadi hatua ya mwisho katika kulinda watoto wetu bila kuogopa vitisho au janga lolote linaloweza kutokea mbele yetu kwa ajili ya watoto.
Nasema hivi kutokana na ukweli kuwa katika siku za hivi karibuni, wapo akinamama wamekuwa wakitesa na kujeruhi watoto wao hata wengine kupoteza maisha, huku wengine wakizaa watoto na kuwatupa ndio maana nasema huyu ni mfano na anafaa kuigwa.

VIA-HABARI LEO