Sunday, February 22, 2015

MILIKI MAENEO YA MADINI KUFUTWA


MILIKI MAENEO YA MADINI KUFUTWA Waziri wa Nishati na Madini,          George Simbachawene

SERIKALI imetangaza kuanza kufuta umiliki wa maeneo yaliyotelekezwa na wachimba madini kote nchini, ikiwa ni pamoja na kunyang'anya leseni zilizoombwa na wachimbaji ambao wameshindwa kuzilipia.


Kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti juzi na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, wakati akizungumza na wananchi katika maeneo ya Mpwapwa Mjini na katika vijiji vya Godegode na Kisisi.

Alisema wamiliki wengi wa leseni wamekuwa wakifika wilayani kufanya utafiti na uchimbaji, lakini baadhi yao wamekuwa wakihodhi maeneo makubwa, ambayo hawayafanyii shughuli yoyote.
"Watu wengi wanaohodhi maeneo makubwa bila kufanya kazi za utafiti na sasa tutafanya upembuzi yakinifu wa leseni za utafiti moja baada ya nyingine na kufuta leseni zote, ambazo wamiliki wake hawafanyi utafiti kama ilivyokusudiwa," alisema.
Alisema mtu anapopata eneo kwa ajili ya utafiti, anatakiwa kila baada ya miezi sita atoe ripoti ya utafiti na iwapo hajagundua madini, anapaswa kunyang'anywa nusu ya eneo aliloomba na akishindwa kabisa, anatakiwa kunyang'anya leseni.
Migogoro Kwa mujibu wa Simbachawene, watu wengi wamekuwa wakitelekeza maeneo hayo bila kufanya utafiti na wananchi wanapoingia kuchimba na kugundua madini, mwenye eneo hujitokeza na kuwazuia wananchi kuchimba kwa madai anamiliki eneo hilo kisheria.
Simbachawene alisema jambo hilo limekuwa likileta mgogoro kati ya wananchi na Serikali yao, kwa kuwa wananchi wanakuwa hawajawahi kumuona mwenye leseni kutokana na kuingia mikataba bila wananchi wa maeneo husika kujulishwa au kutambulishwa mtu huyo ni nani na mipaka ya eneo lake la uchimbaji ni ipi.
"Wenye leseni za ufatiti wafanye utafiti wao kwa mujibu wa sheria, pia naagiza kuwe na programu ya kutambulisha waliopewa leseni kwa ajili ya utafiti na uchimbaji, ili kuondoa migongano inayoweza kujitokeza," alisema.
Leseni zilizotelekezwa Simbachawene pia alisema Serikali itafuta leseni zote za wachimbaji ambao waliomba, lakini wameshindwa kulipia na kuchukua leseni hizo.
Alisema mkoa wa Dodoma pekee kuna maombi zaidi ya 1,500 ya leseni, lakini wahusika wameshindwa kulipia na kuongeza kuwa kutochukuliwa kwa leseni hizo, ni kuikosesha Serikali mapato.
"Natoa miezi mitatu, watu waende wakalipie leseni zao, mpaka Mei atakayeshindwa kulipia tutazifuta leseni hizo na watapewa watu wengine, hili ni agizo kwa nchi nzima," alisema.
Akizungumzia juu ya miradi ya umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Simbachawene alisema Serikali imedhamiria kupeleka umeme vijijini ili kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora.
Alisema upatikanaji ya umeme vijijini utaongeza ajira kwani watu watakuwa na uwezo wa kumiliki viwanda vidogo. Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye, alisema mpaka sasa wananchi 1,238 katika vijiji 19 wameshaunganishiwa umeme kupitia miradi ya Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) na Rea.
Alisema kati ya hao, wananchi 635 kutoka vijiji wamepata umeme kutoka miradi ya MCC na wananchi 603 kutoka vijiji vinane, wamepata umeme kutoka mradi wa Rea.
Mbali na wananchi, Waziri Simbachawene alisema pia kuna taasisi zilizonufaika na miradi hiyo ikiwemo shule, zahanati, makanisa na misikiti.