Sunday, February 22, 2015

ASKARI WALIOKOSA AJIRA JKT WATAKA UCHUNGUZI HURU UFANYIKE



ASKARI WALIOKOSA AJIRA JKT WATAKA UCHUNGUZI HURU UFANYIKE
Ikiwa imepita siku moja baada ya Mwenyekiti wa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokosa ajira, George Mgoba, kueleza jinsi alivyotekwa na kuteswa, wenzake wameibuka na kutaka uchunguzi huru ufanyike kubaini sindano aliyochomwa kama ilikuwa na sumu.


 
Mgoba ambaye alitekwa Jumatatu iliyopita na kutelekezwa kwenye moja ya mapori mkoani Pwani, juzi ndugu zake walilazimika kumhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi akitokea Amana.
 
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa vijana hao, Parali Kiwango, alisema wanachotaka kujua ni sumu aliyochomwa mwenzao na hatua zitakazochukuliwa.
 
Kiwango alisema kwa sasa wanataka kusimamia matibabu ya mwenzao na kuchagua sehemu ya kumfanyia uchunguzi ili kuzuia serikali kuficha baadhi ya ripoti.
 
Alisema mpaka sasa haijafahamika sindano hiyo ilikuwa na nini.
"Tunachotaka sisi kama viongozi na polisi tushirikiane kuteua hospitali huru ya kuchunguza afya ya mwenzetu, lakini polisi wamekuwa wakituzuia kushiriki kwenye hilo tunaona kunausiri unaoendelea,"alisema.
 
Akielezea kuhusu hali ya Mgobba, alisema bado siyo nzuri na kwamba tayari alishachukuliwa sampuli mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi.
 
"Tumeambiwa vipimo vinafanywa nje ya Muhimbili, lakini hatujui ni hospitali ipi, ubinafsi huu tulianza kuuona kutoka Hospitali ya Tumbi tulipotaka kumchukua walitukatalia walitugomea na wao kutudanganya wanampeleka hospitali kumbe walimleta kituo cha Polisi Kati kwa mahojiano zaidi," alisema.
 
KUTOA TAMKO LEO
Kiwango alisema leo wamekusudia kutoa tamko rasmi kuhusu mwenendo mzima wa sakata hilo kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali kukwepa kusema ukweli kuhusu madai yao ya ajira.
 
Alisema kwa sasa maisha yao yapo hatarini baada ya kuwapo kwa watu wanaowafuatilia majumbani kwao na kila wanapokwenda.
"Kwa jumla hatupo salama tunawaomba Watanzania waelewe hivyo, sisi tunadai haki yetu halali," alisema.
 
CHADEMA CHAZUNGUMZIA
Naibu Katibu Mkuu wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Mnyika alisema mara zote jeshi la polisi limekuwa likisema uongo dhidi ya matukio ya utekaji na uteswaji wa watu.
 
Alikumbusha baadhi ya matukio ya utekwaji na uteswaji na ushambuliwaji wa baadhi ya watu ambao ni  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kutekwa na kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri wa Kampuni ya magazeti ya New Habari, Absalom Kibanda, ambayo alisema hadi sasa Serikali imekuwa na kigugumizi.
 
Mnyika alisema baada ya kupata taarifa dhidi ya tukio la mwenyekiti wa vijana wa JKT, alipiga simu kwa jeshi la polisi ili kujua kiini chake, lakini hawakumweleza ukweli.
 
Mbunge huyo wa jimbo la Ubungo aliihoji Ikulu kwa nini mambo yanayoihusisha ofisi hiyo yamekuwa yakisababisha watu kutekwa.
 
Pia aliihoji serikali kwa nini watekaji hao wamekuwa wakikihusisha chama hicho na vitendo vyao vya kiutekaji kwa kuwahoji wahusika kama wametumwa na Chadema au viongozi wake.
 
MIKOA YAUNGANA KUCHUNGUZA
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia gazeti hili jana kuwa, upelelezi wa tukio hilo la kutekwa na kuteswa kwa Mgoba, utahusisha mkoa wake wa kipolisi na mkoa wa Pwani.
 
Kamanda Kova alisema mikoa hiyo imekubaliana kufanya uchunguzi wa pamoja wa kina kuhusiana na tukio hilo ambalo lilihusisha Dar es Salaam alikotekewa mtu huyo na Pwani alikoteswa.
 
"Tumeanza uchunguzi na mara utakapokamilika basi tutaueleza Umma, tunaomba utulivu wakati hili likiendelea," alisema.
Miongoni mwa madai ya vijana hao ni kupata ajira katika vikosi mbalimbali vya kijeshi kutokana na mafunzo waliyopatiwa.
mwisho