Thursday, December 18, 2014

TATIZO LA WAMACHINGA NA OMBA OMBA MAENEO YASIYORUHUSIWA DAR KUTAFUTIWA DAWA .


TATIZO LA WAMACHINGA NA OMBA OMBA MAENEO YASIYORUHUSIWA DAR KUTAFUTIWA DAWA .
 
unnamed
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki akifuangua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es salaam (RCC) leo jijini Dar es salaam.Kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando.
……………………………………………………………………………………………..
 Aron Msigwa –MAELEZO
.Dar es salaam.
 
Jiji la Dar es salaam linaangalia upya utaratibu wa kuwaondoa ombaomba na wafanyabiashara ndogondogo(wamachinga)  katika maeneo yasiyoruhusiwa katika jiji la Dar es salaam kufuatia sheria na hatua zinazochukuliwa ikiwemo kuwarudisha ombaomba hao katika mikoa wanayotoka kutokuzaa matunda na kuwa endelevu kufuatia wengi wao kurudi katika maeneo ya awali kila wanapoondolewa.
 Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Mecki Sadiki wakati akifuangua kikao cha wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es salaam (RCC) kilichofanyika leo jijini Dar es salaam kujadili masuala mbalimbali ya mendeleo katika jiji la Dar es salaam.
 Amesema kuwa kuendelea  kuwepo kwa wafanyabiashara hao katika maeneo yasiyo rasmi ni moja ya changamoto inayolikabili jiji la Dar es salaam kutokana na biashara wanazozifanya kuchangia kuzuia maeneo ya barabara ya waenda kwa miguu, kusababisha uchafuzi wa mazingira,kusabisha msongamano wa magari kwa baadhi yao kuweka bidhaa  barabarani.
 
Amesema kutokana na hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara walio na biashara rasmi  ambao hulipa kodi za Serikali wamekuwa wakilamikia hali  ya ukwepaji wa kodi inayofanywa na wafanyabiashara hao.
 
Bw. Sadiki amesema mpango wa mkoa wa sasa ni kuendelea kuwatumia wafanyabiashara hao kama  fursa ya mtaji wa rasilimali watu ambayo itatumika kama chanzo cha mapato katika kuleta maendeleo ya mkoa.
 
Amesema watendaji na viongozi wa halmashauri za mkoa wa Dar es salaam wanalojukumu la kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao na kuwatumia katika shughuli za uzalishaji kwa utaratibu mzuri utakaowekwa ili waendelee kunufaika na shughuli wanazofanya.
 
Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za Maji, Elimu na Afya katika jiji la Dar es salaam  amesema kuwa Serikali inaendelea kuzijengea uwezo shule kwa kuongeza majengo ya madarasa, maabara na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaofaulu elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na masomo ya Sekondari.
 
Kuhusu huduma za afya amesema kuwa mkoa unaendelea na maandalizi ya ujenzi wa jengo la ghorofa nane, eneo la Magomeni katika manispaa ya Ilala litakalotumika kutolea huduma ya Afya ya Mama na Mtoto na kuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 500.
 
"  Sasa tuko kwenye maandalizi ya ujenzi wa jengo maalum la kutolea huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika jiji la Dar es salaam litakalogharimu zaidi ya shilingi bilioni ishirini na moja, tayari benki ya Tanzania Investment Bank imeshakubali kutoa mkopo kwa ajili ya jengo hilo" Amesisitiza.
 
Aidha, katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ametoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima  Desemba 14 mwaka huu na kueleza kuwa baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es salaam ambayo uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vurugu, uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku saba.
 
Ameeleza kuwa katika mkoa wa Dar es salaam uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika kwenye mitaa 561 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ulifanyika kwenye mitaa 491 na kuahirishwa kwenye kata 70.
 
Amelitaka jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa linaimarisha ulinzi na usalama wakati wa marudio ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika ndani ya siku 7 katika mitaa yote ambayo uchaguzi uliahirishwa