Wednesday, November 26, 2014

DKT IZAC MARO WA CLOUDS FM AMLILIA JACK WA NJIAPANDA ALIYEUWAWA KIKATILI NA WATU WASIOJULIKANA HIVI KARIBUNI



DKT IZAC MARO WA CLOUDS FM AMLILIA JACK WA NJIAPANDA ALIYEUWAWA KIKATILI NA WATU WASIOJULIKANA HIVI KARIBUNI
JACLINE MASANJA A.K.A JACK WA NJIAPANDA ENZI ZA UHAI WAKE.
 
Ilikua ni miaka kumi iliyopita (10) mwaka 2004, nikiwa ndio kwanza nimeanza kufanya kazi chini ya kaka yangu Dr Sebastian Ndege na chini ya uangalizi wa karibu sana wa boss Ruge Mutahaba na Boss Joseph Kussaga nilipokutana na wewe mdogo wangu Jackline Masanja kupitia Njiapanda ulipokuwa unatafuta msaada ukiwa mgonjwa sana. 

Nakumbuka Dr Sebastian Ndege alipokuona tu alikubaliana na mimi kuwa tuache kila mpango tuliokua nao tuweke nguvu zote kwako. Kweli ulikua unaonekana ni mgonjwa, Kwa kutumia nafasi ya Dr Ndege kipindi hiko akiwa ndio anakaribia kumaliza masomo yake ya udaktari na mimi ndio kwanza nikiwa mwaka wa pili wa udaktari tulifanikiwa kuhakikisha kuwa unapata matibabu ya haraka uliyokua unayahitaji sana. 

Ulikua shujaa sana kukubali kusema kuwa uko tayari Dr Ndege atangaze hali yako mbele ya uma wa WaTanzania na kwa ruhusa yako tukafanya kipindi na wewe huku ukiwa mgonjwa na ukasema kuwa umeathirika na kwa kipindi kile kinga yako ilikua chini sana (CD4 zilikua 4). 

Wewe ulikua ni watu wa mwanzo kabisa kuja mbele ya umma kuongea kuhusu hali halisi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na maradhi ya UKIMWI. Tulikuita shujaa na Muhimbili ulipokua unatibiwa kipindi kile wahudumu wote walikuita Jackie wa Njiapanda (ndio chanzo cha kumuita jina hilo miaka yote hii). Kutokana na juhudi nyingi zilizofanyika ulipona kabisa na ukarudi kwenye hali yako ya kawaida ya kawaida na ukaendelea na maisha yako.

Kutokana na yote yaliyotokea mimi na Dr Ndege tukaona ni vyema kama tutakuomba ukae na sisi kama Njiapanda na uendelee kutusaidia kwa kuwa Njiapanda ilikua imekua sana na waliokua wanahitaji msaada walikuwa wanaongezeka kila kukicha. Hukusita kukubali na kuanzia miaka hiyo ukawa unatusaidia kushughulika na wote wanaohitaji msaada wa Njiapanda. Ni wengi uliwachukua na kukaa nao kwako ingawa hali yako ya kiuchumi haikua nzuri sana kusema eti wewe ni tajiri.

Miaka ilienda na ukaendelea kupambana na maisha huku ukiendelea vyema. Nakumbuka vizuri sana sakata la dawa ya Babu wa Loliondo lilipoanza mimi na wewe tulikua hasi na chanya. Mimi nilikua napinga sana kwa kuwa nilikua na sababu za kisayansi na wewe siku zote ulikua unakasirika kwa kuwa ulikua ukiamini kuwa dawa inaponya. Ukaniomba nikuruhusu uende na kweli tukakubaliana tukafanya mchakato na ukaenda. Tukakubaliana kuwa mimi nachohitaji ni kimoja tu nacho ni kukutumia wewe kama somo kwa hiyo tukarekodi kila kitu kabla hujaenda kwa babu na tukafanya kipindi maalum. 

Ukasema kinga yako ni ngapi na kila kitu wala hukuogopa. Ukaenda Loliondo ukanyweshwa kikombe na ukarudi. Tukafanya kipindi ukasema unaendelea vizuri. Tukaendelea na vipimo na maisha yakaenda. Miezi miwili baadae nakumbuka nilikua nimekaa kliniki nikakuona kwa chini unatembea huku unajikongoja, nikakufuata pamoja na manesi wa pale clinic tukakuchukua tukaendelea na uchunguzi tukagundua kuwa kinga yako imeshuka sana kwa kuwa baada ya kwenda kwa babu hukuendelea na dawa (kinga ilikua 14). 

Tukaanza kufanya jitihada za kuhakikisha afya yako inarudi kuwa nzuri na kweli ukawa Ok na tukafanya kipindi tena kuhusu kilichotokea. Kama kawaida ukawa shujaa na kusema kila kitu. Kupitia kwako waTanzania wakajifunza mengi kuhusu kikombe cha babu na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa ujumla. Kupitia wewe Jackline Masanja watu wakafanya maamuzi huku wanajua, ambayo kisayansi ni jambo la maana sana. Jackie mdogo wangu, mimi na Dr Sebastian Ndege kamwe tusingeweza kuifikisha Njiapanda ilipofika bila ya ushujaa wako, bila ya utayari wako wala bila ya uwazi wako. 

Sio tu kwa kupitia story yako watu wamejifunza mengi kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI bali pia mchango wako wa kusaidia Njiapanda na watu wa njiapanda tumeweza kufanya mengi sana. Nakumbuka habari ya wamasai uliileta wewe, habari ya yule msichana aliyelazimishwa kufanya mapenzi na mbwa ilitoka kwako, watoto wa mitaani wanaolazimishwa kufanya mapenzi kinyume cha maumbile pale kariakoo uliifuatilia wewe mpaka ukalala kariakoo usiku kucha kuifuatilia. Ni nyingi sana Jackie.

Jackie, kwangu mimi na kwa Dr Sebastian Ndege wewe ni mdogo wetu yule yule wa miaka 10 iliyopita. Ulikua unatuita kaka na sisi tukauita mdogo wetu. Nakumbuka hata mambo yalipokua magumu nikgombana na ma boss wangu kina Ruge nilikua nakuomba ukaniombee msamaha maana boss Ruge alikua anakupenda sana kama mdogo wake, nilijua kuwa ukisema tu boss atanisamehe hahahaaaaa…asante sana mdogo wangu kwa kuokoa jahazi mara kwa mara lol.

Leo hii nimeamua kuandika huu waraka mrefu kwako wewe Jackie kwa kupitia ndugu zangu wa Facebook na platforms nyingine kwa sababu, siku ya jumamosi 22 November 2014 nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu Geah Habibu kukuhusu wewe mdogo wangu, kwamba mwili wako umekutwa ukiwa umekwishafariki. 

Sio tu kuwa kifo chako kilikua cha kawaida bali inaonekana umeuawa. Kwa bahati mbaya sana kwa sasa siko nchini kwa hiyo sikuamini na sikuweza kufanya chochote mpaka pale nilipoona picha yako. Kusema ukweli bado sikuamini so nikaongea na Douglas na Amani (watengenezaji wa Njiapanda) wafuatilie hii habari. Mwisho wa siku ni kweli ikaonekana kuwa umeuawa tena kikatili. 

Nikawasiliana na kaka yangu Dr Sebastian Ndege naye hakuamini. Jumapili ilipofika nikasema nisiseme chochote maana naona bado si kweli (nisamehe mdogo wangu) nikajikaza nikafanya Njiapanda bila kusema chochote. Jana jumatatu ndio Geah akanihakikishia kuwa ni kweli umefariki na baba yako amekutambua na msiba kweli uko.

Nimelia sana, sijui kwa nini umefanyiwa ukatili huu, siwezi kusema chochote kwa kuwa sijui, lakini kitu kimoja nachoamini na kinachoniuma moyoni mwangu ni kuwa mimi, wewe na Seba tumepambana sana Zaidi ya miaka kumi kuhakikisha unakua ok na afya njema, najiuliza swali yote hiyo ilikua kwa nini? JE NI KWELI KUWA JUHUDI ZOTE HIZO ZILIKUA KUKUTAYARISHA UJE UUWAWE KINYAMA NAMNA HII??

Mwenyezi Mungu pekee ndie anayejua kilichotokea na ndiye anayejua hukumu ya kila mmoja wetu. Jackie mdogo wangu umeenda, umeacha wadogo zako na familia yako. Mungu akulaze mahali pema peponi mdogo wangu, naamini sasa utapumzika maana umehangaika sana na haya maisha.

Familia yako naamini Mungu atabariki itakaa salama na yote yatakua heri. Dr Ally Kaduma na clinic nzima ya IDC wanakulilia, Clinic ya watoto na ya watu wazima ya DarDar wanakulilia watamiss unga wako ule wa uji wa watoto uliokua unaleta.

Clouds Media yooote inakulilia, boss Ruge anakulilia, familia yote ya Njiapanda inakulilia, kina mama Derick na kina brother Gelvas na kaka yako mkubwa kabisa Danny Kiondo wanakulilia.

Mimi, Dr Ndege, Mishy Singano, Jackie Chengula (tunamwita JACKIE mkubwa kwa kuwa wewe ulikua unajiita Jackie mdogo), Simon Simalenga, Amani Siri, Douglas Pius, Arnold Kayanda (hadi harusi yake ulisimamia), Geah Habib, Regina Mwalekwa, Ruge Mutahaba, Team Njiapanda ya tangu 2003 mpaka ya leo wote tunakulilia mdogo wetu. 

Kwetu sisi wote wewe bado ni Jackie wa Njiapanda yule wa tangu 2004. Mdogo wetu mwenye upendo na uliyekua tayari kutumia hadithi ya maisha yako kama fundisho kwa wengine. Wewe ni shujaa na kamwe hilo halitokaa libadilike. Sheria itachukua mkondo wake kwa wote waliosababisha kifo chako na Mungu atamhukumu kila mtu kwa jinsi alivyotenda.

Ninalia sana, ninahuzunika sana ninatamani ningeweza kufanya lolote lakini nimeshindwa ndio maana nikashindwa kukuokoa na hili, Mungu atanisamehe maisha yameniweka mbali na wewe mdogo wangu mpaka mauti yamekukuta. Kibaya Zaidi ni kuwa hata kukuzika sitaweza kwa kuwa niko mbali na nyumbani. Lakini ninaamini huko ulipo utafurahi kufahamu kuwa ninafanya yote haya ninayofanya ili niweze kuwasaidia waTanzania wenzetu vizuri Zaidi nao wawe na afya njema kama nilivyojitahidi kufanya yako iwe.

Ulale pema peponi mdogo wangu, Jackline Masanja..
Mungu ibariki familia yako,
Mungu ibariki Clouds Media Group
Mungu ibariki Njiapanda