Sunday, July 27, 2014

MBATIA AONGOZA MAZISHI YA KAMISHINA NCCR

 

MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi James Mbatia akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Kamishina wa chama hicho mkoa wa Mara Stephine Sebeki Kijiji cha Nyamilema wilayani Serengeti,kulia ni Katibu Mkuu wa NCCR Moses Nyambabe.Picha na Shomari Binda
 
NA SHOMARI BINDA-SERENGETI
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia ameongoza wananchi wa Wilaya ya Serengeti kwenye mazishi ya aliyekuwa Kamishina wa Chama hicho mkoa wa Mara Stephine Sebeki katika Kijiji cha Nyamilema baada ya kuuwawa julai 22 kwa kukatwa mapanga.
 
Akitoa salama za rambirambi za chama hicho,Mbatia ambaye aliongoza na viongozi mbalimbali wa chama pamoja na wabunge wanaotokana na chama hicho,alisema walikipokea kifo cha Sebeki kwa masikitiko makubwa kutokana na tukio lililopelekea kifo chake na kudai ni lazima Serikali ione namna ya kukabiliana na matukio ya mauaji.
 
Alisema Sebeki ambaye alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mageuzi tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992 amekatishwa uhai wake kwa tukio la kinyama na kutumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii ya mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla kujitambua na kuachana na matukio ya mauaji.
 
Mbatia alisema hata Sheria ya wanyama hairuhusu kumchinja ng'ombe ama mbuzi huku mnyama mwingine akiwa anaangalia lakini hii leo watu wameingiwa na shetani na kufanya matukio ya mauaji mchana na kusema kuna kila sababu kuona hali hiyo haitokei ili jamii iendelee kuishi kwa amani.
 
Mwenyekiti huyo wa NCCR ambaye muda wote alikuwa akiongea kwa uchungu kufuatia kifo cha kiongozi huyo,alisema kutokana na taarifa za kuwepo kwa matukio ya mauaji wilayani Serengeti kuna kila sababu uongozi wa halimashauri kukaa na kuona namna ya kukomesha matukio hayo na kuacha kuishia kutoa pole kwenye misiba.
 
Alisema kutokana na kukatishwa uhai wa kiongozi huyo ambaye ameacha mjane na watoto 7 atahakikisha inafunguliwa akaunti ya elimu kwaajili ya watoto wa marehemu ili waweze kusoma na kutambua thamani ya uhai na kuwapunguzia unyonge.
 
"Akaunti hii ambayo mimi mwenyewe ntahakikisha kwa kushilikiana na Katibu Mkuu wa NCCR inafunguliwa ntaichangia milioni 5 lakini pia kwenye vikao vya chama ntawaomba viongozi wengine wachangie milioni 5 ili tuweze kuanza na milioni 10 ya kuwezesha elimu ya watoto wa marehemu,"alisema Mbatia.
 
Kwa upande wake Mbunge wa Afrika Mashariki na Katibu wa Mambo ya Nje wa NCCR Mageuzi Nderakindo Kessy alisema kuna kila sababu ya kuandaliwa sheria hata wale wanaomiliki sime ama mapanga kuweza kusajiliwa na kufatiliwa matumizi yake.
 
Viongozi wengine walioambatana na Mbatia kwenye mazishi hayo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa NCCR Ghati Musore,Katibu Mkuu Mosena Nyambabe,Mbunge wa Kasuru Vijijini Anglepina Buyogera(NCCR-Magezi) pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa hapa nchini.